WAGANGA WA JADI ACHENI KUWA CHANZO CHA MAUAJI YA ALBINO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 2 December 2020

WAGANGA WA JADI ACHENI KUWA CHANZO CHA MAUAJI YA ALBINO


Pichani walemavu wa ngozi ambao Waganga wa Jadi wametakiwa kutokuwa chanzo cha mauaji yao na kuhakikisha wanawakinda kea nguvu zao zote


WAGANGA WA TIBA ASILI nchini wametakiwa kutokuwa chanzo cha mauaji ya wazee na watu wenye ulemavu wa ngozi Albino,bali wawe ni sehemu ya kuwalinda wasiuwawe.

Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa dawati la Jinsia, wilaya ya Moshi, Mkaguzi wa Jeshi la Polisi, Erina Maro, kwenye hafla fupi ya waganga hao kutoa zawadi ya vyakula,sabuni ,sukari na mafuta ya kupikia kwenye kambi ya kutunzia wazee iliyopo  Njoro manispaa ya Moshi.

Alisema kuwa hakuna mtu mwenye haki ya kutoa uhai wa mtu mwingine ,hivyo waganga wahakikishe tiba wanazozitoa hazisababishi vifo vya wazee hasa wenye macho mekundu yanayosababishwa na matumizi ya kuni.

Maro,amewaambia waganga hao kutoa tiba zao kwa  kutambua kuwa wazee wanayo haki ya kulindwa kama watu wengine na wao pia ni sehemu ya jamii.

Amewataka waganga hao kuhakikisha wanaendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kuwafichua waganga ambao wanaendesha tiba zenye ramri chonganishi zinazosababisha wazee na Abino kuuliwa.

Akawataka  wajisafishe kwa kuacha kutoa matibabu ya kuzindika majambazi na wahalifu ili wasikamatwe na polisi pindi wanapofanya uhalifu.

Akikabidhi misaada hiyo mkurugenzi wa Chama cha waganga wa tiba asili na wakunga wa jadi, TATDM, Nyaki Daudi, amesema kuwa waganga hao ambao walikuwa na kongamano lao la siku kumi lililofanyika kijiji cha Mabungo ,wilaya ya Moshi vijijini ,wameamua kutoa misaada yao kwa wazee walioko kambini hapo kutokana na kutambua uhitaji wao.

Alisema kuwa waganga hao walikutana kwa ajili ya kukomesha mauaji ya wazee na Albino pamoja na kukomesha tiba zinazoandamana na ramri chonganishi zinazosababisha vifo vya wazee na Albino.

Naye mkuu wa kituo hicho Josephine Kesy, ambae ni afisa ustawi wa jamii, amesema kuwa Kambi hiyo ambayo ni ya serikali inao jumla ya wazee 15 kati yao wanawake ni wane.

Alisema kambi hiyo inapokea wazee hao ambao zamani walikuwa wakifanya kazi kwenye mashamba makubwa na mara baada ya mashamba hayo walikosa pa kwenda kwa kuwa hawajui makwao kwa kuwa walizaliwa kwenye mashamba hayo na wengine walifika wakiwa ni wadogo.

 

No comments:

Post a Comment