TANGAWIZI YAWAINGIZIA WAKULIMA WA MADABA SONGEA ZAIDI YA BILIONI MOJA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 7 December 2020

TANGAWIZI YAWAINGIZIA WAKULIMA WA MADABA SONGEA ZAIDI YA BILIONI MOJA

 

zao la tangawizi

WAKULIMA wa Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma wamepata zaidi ya shilingi bilioni moja kutokana na mauzo ya zao la tangawizi katika kipindi cha mwaka 2019/2020.

Afisa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri hiyo Joseph Mrimi akizungumza ofisini kwake mjini Madaba,amesema kutokana na mauzo hayo  Halmashauri imeingiza zaidi ya shilingi milioni 16 ambazo ni mapato ya ushuru sawa na asilimia tatu ya mapato .

Mrimi amesema uzalishaji wa tangawizi katika Halmashauri hiyo msimu huu umefikia tani 5,117 ambazo zimeuzwa  ndani na nje ya Nchi.

“Halmashauri ya Wilaya ya Madaba tumeweka mkakati wa kuongeza  thamani ya zao hilo na kuongeza uzalishaji zaidi wa zao hilo ambalo soko lake hivi sasa ni kubwa’’,alisisitiza Mrilimi.

Amesema Halmashauri imetenga jumla ya Hekari 400 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali vya kuchakata mazao ya kilimo ikiwemo zao la tangawizi.

Kwa upande wake Mchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Bosko Komba amesema,Halmashauri ya Wilaya hiyo imechukua hatua mbalimbali za kulitangaza zao hilo  katika maonesho ya wakulima nanenane Kanda ya Mbeya na Maonesho  ya Uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma.

Amesema tayari Kampuni ya TANZANICE imeahidi kununua tangawizi toka kwa wakulima wa Madaba ,na kwamba matarajio ya Halmashauri siku zijazo ni kupata msindikaji mkubwa.

Hata hivyo amesema Halmashauri imejipanga kuwahamasisha wakulima  wanaoweza kulima na kusindika zao hilo ambapo amejitokeza Mkulima mmoja toka Kijiji cha Ifinga kulima na kusindika zao hilo.

Amesema ni azma ya Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na  wadau mbalimbali kununua na kusindika tangawizi  ili zao hilo liendelee kuongeza uchumi wa Madaba na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment