TAJIRI SUBHASH PATEL KUZIKWA ALHAMISI DAR, WAZIRI MKUU MAJALIWA 'AMLILIA'...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 15 December 2020

TAJIRI SUBHASH PATEL KUZIKWA ALHAMISI DAR, WAZIRI MKUU MAJALIWA 'AMLILIA'...!

Tajiri, Subhash Patel


MFANYABIASHARA maarufu na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni ya Motisun Group, Subhash Patel amefariki dunia Jumanne Desemba 15, 2020 na tayari familia ya Patel imetangaza kuwa anatarajiwa kuzikwa Alhamisi makaburi ya Wahindu Makumbusho jijini Dar es Salaam. Tajiri huyo ambaye alikuwa mgonjwa amefariki nyumbani kwake maeneo ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametuma salaam za rambirambi kutokana na kifo cha Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya Motisun Group, Bw. Subhash Patel kilichotokea leo jijini Dar es Salaam. “Hayati Shubash, ana mchango wake kwenye sekta ya viwanda, alikuwa rafiki wa wote, mcheshi, ametoa msaada kwa maskini na matajiri na hakuwa mbaguzi,” amesema Waziri Mkuu wakati akimuelezea Bw. Patel. “Ninatoa pole kwa wanafamilia, ndugu na wote walioguswa na msiba huu. Taifa limempoteza mmoja wa wazalendo wake. Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina.”

Katika salamu alizozitoa Desemba 15, 2020, Waziri Mkuu amesema amehuzunishwa na kifo cha mfanyabiashara huyo maarufu nchini ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) na mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF). Mmoja wa wanafamilia amesema, Bw. Patel amefia nyumbani kwake, Kisutu jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akiendelea na matibabu na anatarajiwa kuzikwa keshokutwa (Alhamisi, Desemba 17, 2020) kwenye makaburi ya Wahindu yaliyoko Kijitonyama, Dar es Salaam.

Mfanyabiashara huyo maarufu nchini alikuwa akimiliki kampuni zinazotengeneza bidhaa za plastiki, saruji, mabati, nondo, nyaya za umeme, vinywaji, rangi na pia alimiliki hoteli za White Sands na Sea Cliff, Pearlsun Hotel & Resorts.

Kampuni ya Motisun inamiliki hoteli maarufu nchini Tanzania za White Sands na Sea Cliff na ndio wazalishaji wa juisi na maji chapa ya Sayona, saruji chapa Mamba. Bidhaa nyingine maarufu ni rangi, mabati na matangi ya kuhifadhia maji ya chapa Kiboko. Kampuni hiyo pia ina mtandao wa biashara nchini Msumbiji, Zambia na Uganda.

No comments:

Post a Comment