Waziri Mkuu Kassim Majaliwa |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na
Biashara ikamilishe utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji ili kuuwezesha
kila mkoa kujua bidhaa hiyo inapaswa kuuzwa kwa bei gani kwa nia ya kuondoa
upandishwaji holela unaofanywa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.
Pia, Waziri Mkuu ametoa onyo kwa mawakala wa saruji kutoficha
bidhaa hiyo kwa lengo la kupandisha bei kwa sababu kitendo hicho ni sawa na
uhujumu uchumi, hivyo watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa
sheria.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Desemba 7, 2020 alipozungumza na
Wakuu wa Mikoa, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Uchukuzi, Maafisa Biashara wa Mikoa, Mawakala wa saruji walioko
mikoani na Wakurugenzi wa viwanda vya saruji. Kikao hicho ambacho Waziri Mkuu
alikiongoza kwa njia ya televisheni akiwa ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma
kilihusu suala la bei na mwenendo wa upatikanaji wa saruji.
Waziri Mkuu amesema lazima utaratibu wa kuwa na bei kikomo ya saruji
ukamilike ili kujua kila mkoa bidhaa hiyo inapatikana kwa kiasi gani. “Mfano
saruji inazalishwa Tanga au Dar es Salaam alafu Morogoro inauzwa kwa shilingi
28,000 sasa Kigoma itauzwaje lazima kuwe na bei kikomo.”
Ameongeza kwa kusema kuwa suala hilo halihitaji kuundiwa bodi
kwa sasa kwani vyombo vya kusimamia biashara vipo, wizara husika ipo, hivyo
amewataka wahusika wote wahakikishe wanasimamia suala hilo kikamilifu ili
kuwawezesha wananchi kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuiagiza Tume ya Ushindani (FCC)
ifanye ukaguzi ili kubaini kama bei za bidhaa hiyo ni shindani na zina tija kwa
wananchi kwa sababu katika maeneo mengine hazina uhalisia na zinasababisha
usumbufu nchini.
“…Mawakala badilikeni na acheneni na tabia ya kuficha bidhaa kwa
ajili ya kuzipandisha bei, ukikutwa unatengeneza mazingira ya kuifanya bidhaa
isipatikane kwa lkengo la kuipandisha bei huo ni uhujumu uchumi. Ukikamatwa na
bidhaa ambayo inatafutwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yako.”
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Wizara ya Viwanda na
Biashara watembelee viwanda mbalimbali ili kusikiliza matatizo yanayowakabili
wenye viwanda na kushirikiana nao katika kuyapatia ufumbuzi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema licha ya bei ya saruji kuanza kupungua
nchini, amewataka wakuu wa mikoa waendelee kufanya ukaguzi na kufuatilia
mwenendo wa bei ya saruji ili kubaini kama bei wanayouziwa wananchi ni halali
na wahakikishe bei ya bidhaa hiyo inaendelea kushuka.
Amesema viwanda vya saruji havina budi kupanua wigo kwa kuwa na
mawakala wengi hadi vijijini ili kumudu kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa
sababu mahitaji ya saruji nchini ni makubwa kwani Watanzania wanaboresha makazi
yao kwa kujenga nyumba bora hadi vijijini.
Licha ya bei ya saruji kuanza kushuka katika mikoa mbalimbali
nchini, imeelezwa kuwa katika baadhi ya mikoa kama Dodoma, Ruvuma, Simiyu,
Tabora bado upatikanaji wa bidhaa hiyo hauridhishi na inauzwa kwa bei kubwa.
No comments:
Post a Comment