MAJALIWA: VIONGOZI WA USHIRIKA LAZIMA MBADILIKE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 1 December 2020

MAJALIWA: VIONGOZI WA USHIRIKA LAZIMA MBADILIKE



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa vyama vya ushirika nchini wabadilike na wawe weledi ili kurejesha heshima ya ushirika nchini.

 

“Viongozi wa ushirika ni lazima tubadilike. Nyie mliopewa dhamana kwenye vyama vikuu hivi vitatu vya KNCU, NYANZA na SHIRECU lazima mbadilike. Nyie mmepewa dhamana ya kuwasaidia Watanzania wenzetu wanyonge wanaolima ekari moja, mbili au tatu,” amesema.

 

Ametoa wito huo leo jioni (Jumatatu, Novemba 30, 2020) kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Hazina, jijini Dodoma, wakati akizungumza na viongozi mbalimbali waliohudhuria kikao maalum cha kupokea taarifa ya ufuatiliaji wa mwenendo wa vyama vya ushirika vya NCU (1984) Ltd, KNCU (1984) Ltd na SHIRECU (1984) Ltd kutoka kwa timu maalum ya uchunguzi aliyoiunda.

 

Viongozi hao ni Wakuu wa Mikoa sita ya Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Tanga, Geita na Simiyu, Makatibu Wakuu wa Fedha, Ardhi, Kilimo, Viwanda na Biashara, Mrajisi wa Ushirika Taifa, Warajis wasaidizi wa Mikoa, Menejimenti ya Tume ya Ushirika na wajumbe wa Bodi za KNCU, NYANZA na SHIRECU. Wengine ni Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania.

 

“Ninasema viongozi bado hatujabadilika kwa sababu hata suala la usambazaji wa mbegu kwa wakulima badi ni changamoto. Wengine wamekuja kujifunza ushirika hapa nchini na wamesonga mbele lakini sisi hatuendi mbali kwa sababu ya kukosa weledi, uaminifu na uwajibikaji katika majukumu tuliyowakabidhi.”

 

“Nendeni mkasimamie ushirika ili heshima ya ushirika wa zamani wali irejee, hali ya ushirika ule ambao uliacha mali za ushirika. Bado kazi yangu ya hizo mali haijakamilika. Tunataka tuzisimamie na tuwakabidhi kitu ambacho kimekamilika.”

 

Amesema anasikitika kuona kwamba makosa ya ushirika yanafanyika wakati warajis wasaidizi wapo na hata kwenye Halmashauri kuna Maafisa Ushirika. “Haya madudu yanafanyika lakini warajis wa mikoa mpo, na nyie ndiyo wasimamizi wa ushirika. Je mnafanya nini?”

 

“Lazima uhakikishe vyama vya msingi, vinasimamiwa na vinakwenda kama ambavyo sheria yetu ya ushirika inasema. Warajis wasaidizi wapo kila mkoa. Na kila wilaya kuna Afisa Ushirika. Ni kwa nini mambo hayaendi?” alihoji Waziri Mkuu na kuongeza: “Hatutasita kuchukua hatua kali dhidi ya mtu anayehujumu mali za ushirika. Tulianza na tutaendelea kusimamia mali za ushirika.”

 

Mapema, akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, kiongozi wa timu hiyo maalum, Bw. Asangye Bangu alisema timu hiyo imefanikiwa kurejesha mali 60 za ushirika zenye thamani ya sh. bilioni 68.98. “Mali hizo zinajumuisha majengo, viwanja, magari na mitambo ya mashine, hazikuwa mikononi mwa vyama hivi vitatu lakini sasa zimerudishwa kwenye vyama.

 

Alisema kati ya hizo, Nyanza ilikuwa na mali 37 zenye thamani ya sh. bilioni 61.36, SHIRECU ilikuwa na mali saba zenye thamani ya sh. bilioni 3.33, KNCU ilikuwa na mali 10 zenye thamani ya sh. bilioni 2.03 na TCCCo ilikuwa na mali sita zenye thamani ya sh. bilioni 2.2.

 

Kwa niaba ya wenzake, Bw. Bangu alikabidhi taarifa hiyo ikiwa na mapendekezo kadhaa kwa Serikali.

No comments:

Post a Comment