Naibu Waziri wake aweka mkazo kwenye mawasiliano kuwa ni usalama wa nchi
Prisca Ulomi na Faraja Mpina, WMTH
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amekutana na Menejimenti ya Wizara hiyo mara baada ya kuapishwa Ikulu ya Chamwino, Dodoma akiambatana na Naibu wake Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew kwa lengo la kufahamiana na kutoa maagizo juu ya utendaji kazi ili Wizara hiyo mpya isimame na kuchukua nafasi yake katika utoaji wa huduma za Serikali kwa wananchi.
Akizungumza na Menejimenti kwenye ukumbi wa mikutano wa Wizara uliopo Mji wa Serikali Mtumba, Dkt. Ndugulile amewataka watendaji wasisubiri kuagizwa, wafanye kazi kwa bidii ili kabla ya kuulizwa wawe wamejiongeza na kutekeleza.
Aliongeza kuwa, Wizara hiyo ni mtambuka, ya kimkakati na kiuchumi na inagusa Wizara zote na maisha ya kila mtanzania, ina nafasi kubwa na muhimu katika kuchangia pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.
“Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha Wizara inasimama na kuchukua nafasi yake, sisi ndio wenye sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016, sheria, kanuni na miongozo mbali mbali hivyo tunaenda kugusa Wizara takribani zote zinazotumia miumboninu na mifumo ya TEHAMA na huduma za mawasiliano katika utoaji huduma na ukusanyaji wa kodi za Serikali”, alisisitiza Dkt. Ndugulile.
Dkt. Ndugulile amesema tunapoongelea uchumi wa kidijitali ni pamoja na ukuaji wa matumizi ya TEHAMA ambayo dunia inaitambua na kuwekeza katika teknolojia hii muhimu ambayo ina akisi akili za binadamu katika uzalishaji na utoaji wa huduma kwa jamii.
Hivyo, amewataka watendaji wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa bidii huku wakitekeleza masuala yanayohusu Wizara hii mpya kama yalivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025 pamoja na yaliyopo kwenye hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Novemba mwaka huu.
Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Mathew, amesema kuwa Wizara hii mpya imebeba mambo mengi ya kijamii, kiuchumi na usalama wa nchi ambapo mawasiliano yanagusa moja kwa moja usalama wa nchi hivyo ni budi kufanya kazi kwa ubunifu, umakini na weledi mkubwa.
Aliongeza kuwa, changamoto za mawasiliano zipo hivyo tujipange kuzifanyiwa kazi katika mtazamo wa utendaji unaoleta matokeo yanayoonekana badala na wataalamu ambao ni wazungumzaji mahiri na sio watendaji.
“Umefika wakati wa kutumia wataalamu wetu wa ndani kutengeneza mifumo yetu wenyewe, ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii ambayo itatengenezwa na sisi wenyewe kuendana na mahitaji ya wananchi wetu badala ya kukumbatia teknolojia kutoka nje ya nchi, tukijipanga vizuri hakuna kinachoshindikana ili Serikali iweze kuwasiliana yenyewe kwa yenyewe, na wananchi wake na wafanyabiashara kutumia TEHAMA”, alisisitiza Mhandisi Mathew.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa mifumo ya TEHAMA inahitaji watu makini, waadilifu na weledi ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuelekea Tanzania ya kidijitali ili kutafsiri maono ya Mhe. Rais Dkt. Magufuli ya kuunda Wizara mpya.
“Sisi ndio tumepewa dhamana ya kuisimamisha hii Wizara mpya isimame, misingi ipo lakini ili kuleta matokeo chanya inatupasa kuwa wazalendo kwa kuitendea haki nchi yetu kwa niaba ya wengi”, alisema Dkt. Chaula.
No comments:
Post a Comment