Na Mwandishi Wetu Katavi
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Dkt. Jingu amesema vitendo vya watu kuwapa mimba na kuwaoa watoto haviwezi kukubalika kuendelea katika Jamii.
Dkt.Jingu ameyasema hayo leo mkoani Katavi wakati akifungua Kongamano la Kupinga Ukatili lililofanyika katika ukumbi wa Polisi Mkoani Katavi.
Amesema kuwa Serikali imefanya mambo mbalimbali katika kuhakikisha vitendo vya Ukatili wa Kijinsia vinatokomezwa katika Jamii zetu.
Ameyataja mambo hayo kuwa Serikali imeanzisha Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, Uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi za wanawake na Watoto, uanzishwaji Madawati ya Polisi ya Jinsia na Watoto na kuhamashisha jamii kwa kutoa elimu ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.
Aidha Dkt. Jingu amesisitiza kuwa uwepo wa Makazi Bora katika jamii ni moja ya njia ya kupunguza vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hasa dhidi ya Wanawake Watoto na Wazee.
"Ni jukumu letu Jamii kuwalinda kuwatunza wanawake, watoto na wazee dhidi ya vitendo vya Ukatili vinavyoweza kuwakabili" alisema
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Abdallah Mohamed Malela amemuhakikishia Katibu Mkuu Dkt. Jingu kuendeleza Kampeni ya Twende Pamoja Ukatili Tanzania sasa basi kwa kuhakikisha wanatoa elimu kwa Jamii ili kuondokana na vitendo vya Ukatili vinavyotokea katika jamii.
"Huku kwetu wazazi wamejikita katika shughuli za kutafuta kipato na kuacha watoto wanajilea wenyewe hii inapelekea kutokea kwa vitendo vya Ukatili dhidi ya watoto" alisema
Akitoa taarifa fupi kuhusu Kongamano la Ukatili Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia Mboni Mgaza amesema lengo la Kongamano hilo ni kukusanya wadau mbalimbali na kujadili namna bora kupambana na Ukatili na Kutokomeza kabisa.
"Kwa kupitia makundi mbalimbali tutatumia muda kujadili kwa kina kuhusu mbinu bora zitakazowezesha kupambana na vitendo hivi vinavyoikabili jamii zetu" alisema
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Benjamin Kuzaga amesema vitendo vya ukatili vinafanyika sana katika jamii kwa kushirikisha wanandugu hivyo kuwataka kufichua vitendo hivyo ambavyo vinawatesa wanawake na watoto.
Nao baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo wamesema kuwa juhudi zaidi zinahitajika katika kuhakikisha elimu inatolewa katika Jamii ili kupata uelewa wa madhara ya vitendo vya Ukatili katika Ustawi wa Jamii.
Kampeni ya Twende Pamoja Ukatili Tanzania sasa Basi inalenga kutoa elimu kwa wananchi ili kupambanana vitendo vya Ukatili vinavyotokea katika Jamii.
No comments:
Post a Comment