Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha kutoka Benki kuu ya Tanzania - Jerry Sabi akibadilisha fedha za kigeni kwenda za shilingi za kitanzania katika ATM, kuashiria uzinduzi rasmi wa mashine hiyo ya kutolea fedha. Wakishuhudia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna na Afisa Mkuu Teknolojia na Mabadiliko ya Digitali wa NMB – Pete Novat(kushoto)
BENKI ya NMB leo imezindua mashine ya kutolea fedha (Automated Teller Machine - ATM) ya kwanza nchini Tanzania yenye uwezo wa kubadili fedha za kigeni kwenda shilingi za kitazania. Hii ni hatua nyingine muhimu kwa Benki ya NMB ya utoaji huduma kwa Watanzania wanaosafiri kwenda nje na watalii wanaokuja nchini Tanzania.
ATM hizi zitawekwa katika viwanja vya ndege vikubwa nchini ambavyo ni uwanja wa Kimataifa vya Julius Nyerere, Uwanja wa Kilimanjaro na ule wa Abeid Amani Karume, Zanzibar, ili ziweze kutumiwa na wasafiri wanaoingia na kutoka nchini wanaohitaji fedha za Tanzania au za nchi waendako.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna alisema, wateja na wasio wateja wa NMB sasa wanaweza kubadilisha fedha hadi kiasi cha Dola za Kimarekani 2,000 kwa wakati mmoja kwa viwango vya kubadilishia fedha vya Benki ya NMB kwa kujihudumia wenyewe kwa kutumia mashine mpya ya ATM zenye uwezo wa kubadili fedha.
NMB imeanza na Dola za Marekani, Euro za Umoja wa Ulaya na Pound ya Uingereza kubadilisha kwenda shilingi ya Tanzania. Wameanza na aina hizo tatu za sarafu lakini muda sio mrefu wataongeza na fedha za mataifa mengine.
Naye Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha kutoka Benki kuu ya Tanzania - Jerry Sabi aliipongeza Benki ya NMB kwa kuwa wa kwanza kuleta huduma hii nchini ambayo imekuja kutoa suluhisho la upatikanaji wa huduma za fedha za kigeni kufuatia kufungwa kwa maduka ya kubadilishia fedha nchini. Alisema Serikali ilizitaka Benki za Biashara kusaidia na kuhakikisha kuwa huduma za kubadilisha fedha nchini zinapatikana kwa urahisi.
Hii ina maana zoezi la kubadilisha fedha sasa litakuwa rahisi na haraka na hasa pindi mashine hizi zitakapowekwa kwenye viwanja hivi vya ndege.
Benki ya NMB imelifanyia kazi hili kwa weledi na ubunifu mkubwa na sasa wamekuja na suluhu ya teknolojia kuongeza nguvu ya upatikanaji wa huduma hii ambayo imekuwa ikitolewa na matawi yao yote nchini. Hivyo basi, uwepo wa ATM za kubadilishia fedha kutasaidia kuhakikisha kwamba huduma hizo zinapatikana wakati wowote (Masaa 24) na kwa urahisi na usalama zaidi.
No comments:
Post a Comment