Mmoja wa wanachama wa TENMET akiwa katika mjadala na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kwamtoro na Shule ya Msingi Kwamtoro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya juma la elimu, wilayani Chemba. |
Ofisa Utetezi wa TENMET, Nasra Kibukila (katikati) akizungumza na wanafunzi wa Sekondari ya Kwamtoro katika mjadala uliofanyika shuleni hapo. |
Mmoja wa wachokoza mada toka TENMET akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kwamtoro na Shule ya Msingi Kwamtoro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya juma la elimu, wilayani Chemba. |
Mratibu wa Taifa wa TEN/MET, Bw. Ochola Wayoga akitoa zawadi kwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Soya aliyefanya vizuri katika masomo yake, kwenye hafla ya maadhimisho ya Juma la Elimu Tarafa ya Soya. |
Wanachama wa TENMET wakiwa katika ziara ya kutembelea shule zenye changamoto anuai na kushiriki katika utatuzi wa changamoto hizo. |
Mmoja wa wanafunzi kutoka Sekondari ya Soya akishiriki katika mjadala wa elimu na wanafunzi wenzake. |
Mmoja wa wanachama wa TENMET akiwa katika mjadala na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Soya ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya juma la elimu, wilayani Chemba. |
Na Joachim Mushi, Chemba
MTANDAO wa Elimu Tanzania (TENMET) ukiendelea na wiki ya maadhimisho ya Juma la Elimu yanayofanyika wilayani Chemba, umefanya mazungumzo na wanafunzi, wazazi na wadau wa elimu katika Tarafa ya Kwamtoro kushirikishana changamoto mbalimbali za elimu katika maeneo yao na kuangalia namna ya kuzitatua.
Mijadala hiyo uliyofanyika kwa makundi mbalimbali ya wanafunzi kwa wanafunzi, viongozi na jamii imefanyika sambamba na kushiriki shughuli za kujitolea kwa jamii kushiriki katika utatuzi wa kero anuai za elimu katika maeneo hayo.
Mashirika wanachama wa TENMET wamewezesha mijadala hiyo sambamba na kushiriki shughuli za ujenzi wa miundombinu ya elimu pamoja na kuchangia ujenzi. Wakiwa Tarafa ya Soya walishiriki shughuli za ujenzi wa madarasa ya shule shikizi ambayo hutumika kusaidia wnafunzi wanaposhindwa kuvuka Mto Magandi na kwenda Shule ya Msingi Soya kipindi cha masika ambapo mto huo hujaa maji.
Mratibu wa Taifa wa TENMET, Bw. Ochola Wayoga akizungumza katika mjadala shuleni hapo alisema mbali na kushiriki kusaidia shughuli za ujenzi kwa vitendo wametoa mifuko 50 ya simenti ambayo itasaidia kuboresha shule hiyo ya muda (Shikizi).
Wakati huo huo, Ofisa Mawasiliano wa Shirika la Uwezo Tanzania, Bw. Greyson Mgoi mmoja ya wanachama wa TENMET amesema pamoja na shughuli hizo za kuboresha elimu wamegawa zaidi ya vitabu 300 kwa wanafunzi tangu kuanza kwa maadhimisho hayo ikiwa ni kuchochea wanafunzi kujenga uwezo wa kujisomea vitabu vya hadithi.
"...Moja ya dhana tulizokuja nazo ni kitabu cha hadithi ambacho pia umeona tukitoa kama zawadi kwa baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri, kitawasaidia wanafunzi hawa kukuza stadi za kusoma na kinamfaa mwanafunzi wa darasa la kwanza hadi la nne," alifafanua Bw. Mgoi.
Wiki ya Maadhimisho ya Juma la elimu inayoendelea inatarajiwa kufikia kilele chake Agosti 21, 2020 katika viwanja vya Shule ya Msingi Chemba, Wilayani Chemba.
Sehemu ya majengo ya Shule shikizi ya Msingi Magandi, Soya. |
No comments:
Post a Comment