Shehe wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Bw. Suleiman Matitu akitoa neno la shukrani kwa Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Mikoa waliochangia katika ujenzi wa msikiti wa Wilaya ya Chamwino. |
Na Mwandishi Wetu- Dodoma
WAKUU wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wamekabidhi Shilingi milioni 30 ujenzi wa msikiti wa kisasa wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Akikabidhi mchango huo Agosti 27, 2020 kwa niaba ya wakuu wengine wa vyombo hivyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Jenerali Venance Mabeyo amesema kuwa wameguswa na azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwawezesha wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo ya imani .
“Naamini kuwa michango zaidi itaendelea kutolewa ili azma ya kujenga msikiti huu ikamilike kwa wakati”, Alisisitiza Jenerali Mabeyo
Hafla ya Kukabidhi fedha hizo imefanyika pembezoni mwa msikiti wa zamani unapojengwa msikiti huo mpya ambapo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,Jenerali Venance Mabeyo amekabidhi fedha hizo kwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali, Charles Mbuge, ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Suma JKT, inayotekeleza mradi huo.
Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge amesema kuwa kiasi cha Shilingi milioni 142 zimeshachangwa na wadau mbalimbali ili kuwezesha ujenzi wa msikiti huo.
Alipongeza jitihada za kuwafanya watanzania kushikamana bila kujali imani zao kutokana na ushirikiano ulioneshwa na wadau mbalimbali katika kuchangia ujenzi wa msikiti huo.
Kwa upande wa Wakuu wa Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara,nao pia wamekabidhi shilingi milioni 26 kwaajili ya Ujenzi huo.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Mikoa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evaristi Ndikilo amesema kuwa wanaunga mkono juhudi za ujenzi wa msikiti huo zilizoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
Aidha, Pamoja na Fedha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka,amekabidhi shilingi milioni mbili zilizochangwa na kanisa la AICC la mkoani humo.
Kwa upande wake, Sheikh mkuu wa Wilaya ya Chamwino Suleiman Matitu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuchangia ujenzi wa msikiti huo na kuhamasisha wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia.
Aidha, Shehe Matitu aliwashukuru Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa mikoa kwa kuchangia ujenzi wa msikiti huo.
Azma ya kujenga msikiti mpya wa Wilaya ya Chamwino ilianzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni wakati wa ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Katoliki la Mt. Immaculata Chamwino ambapo alizindua kanisa hilo baada ya kuchangia ujenzi wake na ukarabati.
Katika kuendeleza azma hiyo alianzisha harambee ya ujenzi wa msikiti huo ambapo hadi sasa kiasi cha Shilingi Milioni 142 zimeshapatikana.
Ujenzi wa Msikiti huo unatekelezwa na Mkandarasi ambaye ni SUMA JKT na tayari vifaa na malighafi mbambali zimeanza kufikishwa katika eneo la ujenzi ili kazi ya ujenzi iweze kuanza mara moja.
No comments:
Post a Comment