Baba Mzazi wa muathirika wa tukio akiwa na huzuni.
Wana kikundi cha Sauti ya Mwanamke chini ya SPRF, wakiwa na familia ya binti aliyefanyiwa ukatili wa kijinsia, kijijini kwao mangaa.
Na Godwin Myovela, Singida
“Nilizibwa mdomo wangu huku nikiwa nimekandamizwa kwa nguvu shingoni, yule kijana alikuwa ameshika panga na akaniambia endapo nitathubutu kupiga kelele basi atakata shingo yangu, sikuwa na msaada wowote, hatimaye alinibaka...nashindwa kusimulia uchungu na maumivu makali niliyoyapata.”
Ni maneno ya kutia simanzi kwa binti wa miaka 14, mwanafunzi wa darasa la saba wa shule ya Msingi Mungaa (jina limehifadhiwa). Mnamo Januari 2019 akiwa anarudi nyumbani akitokea shuleni, mwendo wa takribani nusu kilometa baada ya masomo yake, ghafla kati ya njia alikutana na kijana mmoja anayeishi kijijini hapo.
Kijana huyo ambaye naye (jina limehifadhiwa) akaanza kumshika-shika huku akimvuta kwa nguvu na kumnyonga mikono yake kumpeleka pembeni ya barabara mahali ambako hapakuwa na watu.
“Nilibaki nikitetemeka na kujikuta nikiishiwa nguvu, sikuweza tena kupiga kelele wala kulia kwasababu nilielekezewa panga, akanibaka! Na baada ya tukio jamaa akatoweka. Ndipo mimi nikapata nafasi ya kujikongoja kuelekea nyumbani huku miguu yangu yote ikiwa inachuruzika damu,” anaeleza Mhanga wa tukio hilo.
Nikiwa njiani huku nikilia kwa uchungu nilijiuliza nitaanzaje kuwaeleza wazazi? Na vipi endapo nitapata ujauzito? Na je kuhusu hatma yangu ya masomo itakuwaje? Kwakweli nilichanganyikiwa sana kupitia tukio lile la kinyama; Lakini baada ya kupita miezi 4 kila kitu kilikuwa wazi”.
Kama alivyotabiri binti, siku ile ya tukio ndivyo ilivyotokea… (siku ileile aliyobakwa ndiyo aliyopata ujauzito). Binti akiwa shuleni alionekana mjamzito na Mwalimu Mkuu aliandika barua kuwaita wazazi wake baada ya kukamilisha hatua zote za kumchukua vipimo, ambavyo vilithibitishwa pasipo shaka na madaktari kuwa binti alikuwa mjamzito.
Wazazi waliitwa shuleni na kuelezwa mabadiliko walioyaona kwa binti huyo na hatimaye walijulishwa kwamba binti yao ni mjamzito, na kwa mujibu wa taratibu za shule hiyo hataweza tena kuendelea na masomo, hivyo warudi naye nyumbani.
“Nilikaa nyumbani hadi nilipojifungua. Nilipata wakati mgumu sana kipindi chote cha ujauzito, na wakati wa kujifungua ililazimika nifanyiwe upasuaji (operation) nikajifungua salama lakini kizazi changu kilionekana kina matatizo hivyo kiliondolewa…hapa sina tena kizazi, kizazi changu kimekwisha-ondolewa,” anasimulia binti huyo wa miaka 14 wakati huo huku akitoa machozi.
Anasema kinachomuumiza zaidi ni pale anapomuona mtuhumiwa aliyemfanyia ukatili ule akiwa huru mtaani, na anaishi kwa furaha bila msaada wala habari yoyote, hakuna hatua yoyote aliyochukuliwa mpaka sasa licha ya tukio kuripotiwa Polisi, na baadaye shauri hilo kupelekwa mahakama ya Utemini mkoani Singida.
“Baada ya kesi hii kuripotiwa kituo kidogo cha Polisi katika kijiji cha Mungaa, na baadaye kupelekwa mahakama ya mwanzo Utemini mjini Singida; kila shauri lilipokuwa likitajwa mahakamani tulijikuta tukihudhuria mimi na wazazi wangu, yule kijana alikuwa hafiki…kwa kweli ilifika wakati na sisi tukaishiwa nauli tukashindwa kuhudhuria hii kesi kila ilipokuwa ikitajwa,” anasimulia huyo binti.
Binti anasema mpaka kufikia tarehe 4 Februari mwaka huu, shauri hilo lilikuwa halijatolewa hukumu yoyote, na yule kijana mpaka sasa yupo huru mtaani huku binti yeye akiwa tayari amepoteza mwelekeo na ndoto zake zote za maisha.
“Kwasasa nafanya biashara ya kuuza kuni, hizi kuni huwa nazifuata umbali wa kilometa tatu kutoka hapa nyumbani huku nikiwa na mtoto mgongoni, nafanya hivi ili kutafuta kipato cha kunisaidia kuweza kumtunza mwanangu; nauza kuni hizi shilingi elfu 2 kwa fungu moja,” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la JIOKOE na UMASKINI ‘SPRF’ (yaani Stars of Poverty Rescue Foundation), katika kutekeleza mradi wa AWARE ndio waliotoa taarifa ya tukio hili. Dkt . Suleiman Muttani, na watendaji wenzake kupitia kikundi cha elimu na hamasa cha mradi wa AWARE dhidi ya matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, maarufu ‘Sauti ya Mwanamke’ katika kijiji cha Mungaa ndio walioibua sakata hilo.
Hata hivyo, Dkt. Muttani anasema wanaendelea kuwasiliana na maofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ikungi, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kisheria vinavyoshughulikia shauri hilo ndani ya mipaka yao, ili kuhakikisha wanamsaidia mhanga aweze kupata haki yake stahiki.
“Mbali na matukio mengine ya aina hii, mpaka sasa shirika letu limeibua matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya jamii takribani 56 yakiwemo masuala ya ubakaji, vipigo kwa wanawake na watoto, mimba na ndoa za umri mdogo na mengine ambayo chimbuko lake ni imani za kishirikina sanjari na mila na desturi zilizopitwa na wakati kama ukeketaji ambao kwa sasa unafanywa kwa siri kubwa kwa watoto wachanga usiku wa manane,” anasema Dkt. Muttani.
No comments:
Post a Comment