NMB YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 15.2 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 19 August 2020

NMB YATOA GAWIO LA SHILINGI BILIONI 15.2

Waziri wa  Fedha na Mipango- Dk Philip Mpango akipokea mfano wa hundi  ya Sh. Bilioni 15.2 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB – Dk. Edwin Mhede (wa pili kutoka kushoto) ikiwa  ni gawio kwa Serikali wakati wa hafla iliyofanyika jana Wizara ya Fedha jijini Dodoma. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB - Ruth Zaipuna na wa pili kutoka kulia  ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango - Mary Maganga na wa kwanza kutoka  kulia ni Msajili wa Hazina - Athumani Mbuttuka.


Waziri wa Fedha na Mipango - Dk. Philip Mpango akimkabidhi mfano wa hundi ya Sh. Bilioni 16 Afisa wa Ubalozi wa Uholanzi nchini - Mathis van Eeuwen (kushoto) iliyotolewa na Benki ya NMB kwa Rabo Bank Group. Wengine  katika picha kutoka kushoni ni Msajili wa Hazina - Athumani Mbuttuka, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NMB – Dk. Edwin Mhede na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo -  Ruth Zaipuna.

BENKI ya NMB imetoa shilingi 15. 2 bilioni kama gawio kwa serikali ambayo inamiliki asilimia 31.8 ya hisa zote ndani ya Benki hiyo. Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 45 ya gawio lililotolewa mwaka uliopita ambazo serikali ilipata Sh10.48 bilioni zilizotokana na faida ya mwaka 2018. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB - Ruth Zaipuna alisema kuwa, fedha zilizokabidhiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana katika mwaka wa fedha 2019 baada ya kuondoa gharama na kodi ambayo ilikiwa shilingi 45 bilioni.


Zaipuna amesema mbia mwingine ni Benki ya Rabo ya nchini Uholanzi ambayo imepata gawio la shilingi 16. 8 bilioni huku shilingi 16 bilioni zikienda kwa wawekezaji wengine ikiwemo taasisi za serikali. Alisema kwa mwaka 2019 licha ya benki kuwa chini ya uongozi wa mpito, lakini iliendelea kufanya vizuri na hata kipindi cha corona bado waliendelea kufanya vizuri kwani katika nusu ya mwaka wa fedha 2020 NMB wameshasajili faida ya shilingi 93 bilioni.


Kwa mujibu wa mtendaji huyo, wameshaanza mkakati wa kuinua kilimo nchini na tayari wamekopesha wakulima shilingi 800 bilioni huku wafanyabiashara wakikopa shilingi 2.2 trilioni. Nyingine ni ununuzi wa madawati 40,000 na kompyuta 1000 zilizotolewa kwa ajili ya kusaidia shule mbalimbali na kuwa wameendelea kuwa benki bora kwenye tuzo za jarida la kimataifa la Euro Money kwa miaka 8 mfululizo.


Akipokea mfano wa hundi hiyo, Waziri wa Fedha - Dk. Philip Mpango alisema kiwango kilichotolewa ni kizuri na kuna matumaini makubwa ya gawio kupanda kwa mwaka huu. Dk. Mpango aliitaja Benki ya NMB kuwa miongoni mwa taasisi zinazofanya vizuri zaidi. 


Awali Mwenyekiti wa bodi ya NMB Dk Edwin Mhede aliahidi Benki hiyo itafanya vizuri zaidi mwaka ujao baada ya kupata Afisa Mtendaji Mkuu kwani alipokuwa akikaimu hakuwa na nguvu zaidi katika maamuzi, Hivyo, wanaamini benki hiyo itaendelea kuwa imara zaidi na kuwa mfano kwa mabenki mengine nchini.


Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Phillip Mpango (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya watendaji wa Benki ya NMB na Wizara ya Fedha na Mipango mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kupokea Gawio kutoka Benki hiyo jijini Dodoma, ambapo kiasi cha  shilingi bilioni 15.2  kimetolewa Serikalini.


No comments:

Post a Comment