NGOs ZATAKIWA KUWEKA WAZI TAARIFA ZA MIRADI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 12 August 2020

NGOs ZATAKIWA KUWEKA WAZI TAARIFA ZA MIRADI

Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Idara ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali Musa Leitura akiwaonesha mwongozo wa uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali washiriki wa kikao cha viongozi wa Mashirika hayo Mkoani Kigoma.


Baadhi ya viongozi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoani Kigoma wakimsikiliza Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Samwel Tenga

(hayupo pichani) wakati wa kikao cha pamoja na viongozi hao.


Na Mwandishi Wetu, Kigoma

MASHIRIKA Yasiyo ya Kiserikali yametakiwa kutoa taarifa za kazi zao kwa jamii ili  kutimiza lengo lake la kuisaidia Serikali kutekeleza miradi ya kuhudumia wananchi.

 

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Samwel Tenga wakati wa kikao cha pamoja na Mashirika hayo na timu ya ufuatiliaji kutoka Ofisì ya Msajili wa NGOS.

 

Amesema lengo kuu la kuanzisha Mashirika siyo tu kujitafutia ajira lakini ni kuangalia pengo lililopo katika kuhudumia wananchi.

 

"Lengo ni kuangalia pengo ili kuhudumia wananchi, kuna Mashirika ambayo yanapata ufadhili lakini changamoto ni mawasiliano kati ya Mashirika hayo na Serikali ngazi ya Halmashauri hadi Mkoa kutokuwa mazuri" alisisitiza

 

Amesema kwa uzoefu wa Mkoa wa Kigoma mawasiliano yamekuwa siyo mazuri kwani kati ya Mashirika 150 yanayotambuliwa, yanayotoa taarifa si zaidi ya Mashirika 10. 

 

"Ni changamoto kwa sababu Serikali ya Mkoa au Wilaya inatakiwa ijue Wadau wake na mchango wake kwa wananchi, kuna suala la kutoa taarifa za miradi inayotekelezwa ila umekuwa na pengo la kutoa taarifa" alisema.

 

Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Musa Leitura amesema Serikali inatambua mchango wa Mashirika katika kuhudumia wananchi.

 

"Tumetembelea baadhi ya Mashirika, tumekuta miradi inaridhisha, kwa maana hiyo tunatambua mnafanya kazi kubwa kuisaidia Serikali" alisema.

 

 

Ameongeza kuwa baadhi ya mapungufu yaliyobainika katika kufuatilia mashirika hayo ni  kutokuwa na Ofisi, kutowasilisha taarifa kwa Msajili, kutokuwa na mpango wa uendelevu wa mradi na kutolipa ada.


Aidha, ameyasisitiza Mashirika kuzingatia sheria ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake na katika kuwahudumia wananchi.

 

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Kigoma Msafiri Mzunusi amesisitiza Mashirika kushirikisha Serikali kuhusu mipango yake kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi.

 

Naye Mmmjaya wadau wa NGOs Mkoani Kigoma Limbu Peter   ameishukuruOfisi ya Msajili wa NGOs kwa zoezi la ufuatiliaji lililosaidia kubaini changamoto mbalimbali, hivyo kuzitatua na kusonga mbele.

 

"Tunawashukuru sana kwa kupambanua masuala mengine ambayo tulikuwa hatuyafahamu ikiwemo suala la uendelevu wa miradi" alisema .

No comments:

Post a Comment