MA – DED KUWAJIBISHWA KUSHINDWA KUSIMAMIA LISHE YA WATOTO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 13 August 2020

MA – DED KUWAJIBISHWA KUSHINDWA KUSIMAMIA LISHE YA WATOTO

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Sumbwanga Dkt. Khalfan Haule  Cheti Maalum baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga  kuongoza katika viashiria vya utekelezaji wa Mkataba wa Afua za Lishe katika Mkoa. 

KATIKA kuhakikisha Mwaka wa Mtoto sambamba na malengo ya Mkataba wa utekelezaji wa afua za lishe yanafanikiwa, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani humo kuhudhuria vikao vya tathmini ya lishe ngazi ya mkoa ili kuweza kujibu hoja zinazowakwamisha kufikia malengo ya mkataba huo hasa wakati huu ambapo nchi inajipanga kufikia uchumi wa juu.

Mh. Wangabo amesema kuwa ni dhahiri kuwa lishe bora katika jamii ni kichocheo cha maendeleo katika nyanja zote za Afya, Kilimo, Elimu, Biashara, na Uchumi,   Hivyo malengo ya maendeleo katika nyanja hizi yataweza kupatikana endapo athari za lishe duni au utapiamlo zitakapodhibitiwa.

“Sasa nchi yetu tumeingia kwenye uchumi wa kati, na tuna malengo ya kufikia uchumi wa juu, sasa hapa tulipo tunaweza tukashindwa kama Watoto wetu watakuwa na lishe duni, lakini pia itakuwa ngumu sana kufikia uchumi wa juu, kama huku chini Watoto wetu watakuwa na utapiamlo. Lazima tupige vita utapiamlo ili malengo yetu, maono yetu ya kitaifa, mikakati yetu yote, na mambo mengine yafanikiwe,” Alisema.

Mh. Wangabo ameyasema hayo katika kikao cha Tathmini ya hali ya Lishe Mkoani humo, vikao ambavyo hufanyika mara mbili kwa mwaka katika ngazi ya mkoa, na mara moja katika ngazi ya kitaifa ambapo Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Waganga wakuu wa mikoa huudhuria ili kutathmini hali ya lishe Kitaifa.  

Aidha, Mh. Wangabo ametaka kikao hicho kirudiwe ili wawepo wakurugenzi wa halmashauri ambao wanaweza kujibu hoja za kushindwa kutekeleza makataba huo na si kuwatuma wawakilishi na hivyo kukwepa kuwajibika jambo litakalosababisha kuwajibishwa endapo hawatahudhuria kikao hicho cha marudio kitakachofanyika mwishoni mwa mwezi wa Agosti.

“Hatuwezi kwenda tunaaibika kule wenyewe hawapo, ndio maana umezungumza suala la kuongeza ushiriki kwenye vikao vya kitaifa, lakini kama hapa hawaji hata kule si watakwepa hivyo hivyo, na hata wakifika kule wakati tumekwishaaibika tutakuwa hatujafanya kitu kwahiyo ni lazima tukamatane hapa hapa, kabla ya kwenda huko mbeleni, kabla ya kile kikao cha mwaka cha nchi nzima ni lazima tuwe tumeshikana vizuri mashati,” Alisema.

Halikadhalika, Mh. Wangabo amewashukuru wadau wa mradi wa Lishe Endelevu ambao umekuwa ukitekelezwa katika Mkoa kwa kuwa msaada mkubwa katika kupambana na Utapiamlo na Udumavu ambao wamechangia Mkoa kufikia hali ya katikati katika utekelezaji wa mkataba huo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Boniface Kasululu wakati akielezea viashiria vinavyohitaji kuwekewa mikakati ili kufikia malengo ya mkataba huo amesema kuwa kiasi cha fedha zinazotolewa kwa shughuli za lishe zinapungua mwaka hadi mwaka huku akitoa mfano wa Mwaka wa fedha 2019/2020 kuwa fedha zilizotengwa kwaajili ya shughuli hizo zilikuwa Shilingi 357,027,077/= huku fedha iliyotumika ikiwa Shilingi 108,254,259/= ambayo ni sawa na asilimia 30.

“Ni muhimu kwa Wakurugenzi kusimamia utoaji wa fedha zilizotengwa kwaajili ya shughuli hii ya kutokomeza utapiamlo na udumavu katika mkoa wetu, pia ni vyema wakurugenzi wakasimamia uwajibikaji wa wataalamu wanaohusika na uratibu na utekelezaji wa shughuli za lishe pamoja na kuwawezesha kufanya shughuli za lishe,” Alimalizia.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Kidemografia wa Afya na Viashiria vya Malaria (Demographic Health Survey and Malaria Indicator) wa mwaka 2015/2016 Ulionyesha Mkoa wa Rukwa una asilimia 56.3 ya Udumavu na Utapiamlo. Na utafiti wa masuala ya Lishe (Tanzania National Nutrition Survey) Kitaifa wa Mwaka 2018 unaonesha kuwa Mkoa una asilimia 47.9 ya Watoto walio na Umri chini ya Miaka mitano waliodumaa.

No comments:

Post a Comment