WAZIRI KAIRUKI APIGIA CHAPUO HIFADHI YA TAIFA YA MKOMAZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 10 July 2020

WAZIRI KAIRUKI APIGIA CHAPUO HIFADHI YA TAIFA YA MKOMAZI

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angela Kairuki akisalimiana na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi -Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi Abel Mtui alipowasili katika hifadhi hiyo kukagua shughuli za uwekezaji, katikati ni Kamishna manadamizi wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Herman Batiho.

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angela Kairuki akiwa ameongozana na Mkuu wa wilaya ya Same, Rosemery Senyamule na Makamishna wa uhifadhi wakielekea katika eneo ambalo kumefanyika uwekezaji wa nyumba za wageni wanaofika kwa ajili ya shughuli za utalii katika hifadhi ya taifa ya Mkoamazi.

Moja ya Nyumba zilizojengwa katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kwa ajili ya malazi kwa wageni wanaofika katika hifadhi hiyo.

Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa Kanda ya Kaskazini Herman Batiho akimjeleza jambo Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angela Kairuki baada ya kutembelea sehemu ya uwekezaji wa nyumba kwa ajili ya malazi kwa wageni wanaofika katika hifadhi hiyo.


Kamishanna Msaidizi wa Uhifadhi aliyekuwa Mkuu wa Hifadhi ya taifa ya Mkomazi, kabla ya kuhamishiwa Uduzungwa Abel Mtui akitoa maelezo kwa Waziri Kairuki kuhusu maeneo ya uwekezaji yaliyoainishwa katika Hifadhi hiyo.

Mkuu mpya wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Kamishna Msaidizi Emanuel Moirana akitambulishwa wakati wa ugeni huo.

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu -Uwekezaji Angela Kairuki akizungumza mara baada ya kutembelea sehemu ya uwekezaji uliofanyika katika hifadhi ya taifa ya Mkomazi.

Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini ,Herman Batiho akikabidhi zawadi ya vikombe vyenye nembo ya TANAPA kwa Waziri Kairuki.

Na Dixon Busagaga, Same

WAZIRI Nchi ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji Angela Kairuki ameliomba Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kuipa upendeleo maalumu Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kama zilivyo hifadhi za Kusini na Magharibi badala ya kuiweka katika kundi la hifadhi za Kaskazini zinazo weza kujitegemea.

Kairuki ametoa ombi hilo wakati wa ziara yake aliyofanya katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kuangalia uwekezaji wa eneo la maladhi kwa ajili ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi wanaofika kwa ajili ya kutembelea hifadhi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kukagua nyumba zilizotengwa kwa ajili ya malazi katika hifadhi hiyo Waziri Kairuki alisema kama wasimamizi wa eneo la uwekezaji, wataendelea kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza miundombinu ya majengo katika hifadhi hiyo,.

“Mmeniambia mna maeneo (Site) karibia Saba, na Tano zimeshapata wawekezaji, bado mbili, tutaendelea kushirikiana pamoja kutafuta wawekezaji ambao watakuja kuwekeza katika maeneo hayo, Rai yangu kwenu, mmeanza na hiki kidogo, ila mna uwezo wa kuweka miundombinu ya jengo,” alisema Kairuki.

“Fedha mnazo, mnaweza kuwekeza kwenye Jengo la malazi ya kutosha kwa vigezo mlivyovisema, na ninafahamu kuendesha wenyewe si kazi nyepesi, ila mnaweza kujenga miundombinu na kisha kutafuta watu wa kuiendesha kama mameneja”.

Alisema “Pamoja na kwamba na sisi tutatafuta wawekezaji wengine, lakini Rai yangu ni kwamba na ninyi, muonyeshe uwekezaji mmoja, halafu mtafute waendeshaji au mameneja, maana duniani unaposikia, mahoteli makubwa yakitajwa, kama Serena, waliojenga si wamiliki, wengine wameweka uwekezaji, halafu wanaokuja kuweka uwekezaji ni mtu mwingine, hivyo nanyi Tanapa mnaweza kufanya hivyo hapa Mkomazi,”

Aidha Kairuki alitumia pia nafasi hiyo, kuitaka Hifadhi ya Mkomazi, kutengeneza kitabu kidogo, kitakachoelezea ndege waliopo katika hifadji hiyo na tabia zake kwa maelezo ya kitaalamu kwa lugha nyepesi, ili watu watakaofika waweze kuwafahamu ndege hao kwa undani.

"Numeambiwa hapa Mkomazi, kuna aina 450 za ndege,sasa nishauri, tengenezeni kitabu kidogo kizuri kinachovutia, kitakachokuwa kinaelezea ndege wote waliopo katika hifadhi hii,tabia zao na maelezo ya kitaalamu kwa lugha nyepesi, ili watu watakaokuja kutembelea, wafahamu anamuona ndege yupi na ni wa aina gani,"


Akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule, alisema hifadhi ya Mkomazi bado inahitaji kutangazwa na kuomba kutafutiwa wawekezaji ambao watawekeza hoteli za hadhi mbalimbali ndani ya Hifadhi na hata Wilaya ya Same, ili kuvutia wageni mbalimbali.


"Mkomazi fursa ziko nyingi, na inawezekana baada ya mradi huu kuanza, wageni wakawa wengi, lakini wapo wageni ambao wanaweza kuja tukawapoteza, kutokana na kukosa hoteli ndani ya hifadhi au Same, hivyo tunaomba tupate wawekezaji wa kuwekeza hapa, hata hoteli za hadhi ya Nyota Tano, maana hifadhi hii inaendelea kukua," alisema Senyamule.


Naye Kamisha mwandamizi wa uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Herman Batiho, alisema katika hifadhi hiyo, pamoja na uwepo wa wanyama mbalimbali, pia kuna aina 450 za ndege wa aina mbalimbali ambao pia wamekuwa kivutio kikubwa cha watalii katika hifadhi hiyo.

Hifadhi ya taifa ya Mkomazi inayopatikana kwenye wilaya mbili za Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga nikiwa na maana ya Same na Lushoto ni hifadhi iliyoanzishwa mwaka 1951 kama pori la akiba lililotengwa kutoka Pori kubwa la Akiba la Ruvu.

Kwa sasa hifadhi hii ni miongoni mwa hifadhi za Taifa 22 zilizo chini ya Shirika la Hifadhi zaTaifa (TANAPA) huku maboresho mbalimbali yakiendelea kufanyika katika hifadhi hii ili kuwavutia wageni wengi zaidi vikiwemo vivutio na miundombinu.

No comments:

Post a Comment