VIVUKO VIPYA KUTATUA CHANGAMOTO YA USAFIRI ZIWA VICTORIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 1 July 2020

VIVUKO VIPYA KUTATUA CHANGAMOTO YA USAFIRI ZIWA VICTORIA

Muonekano wa hatua za ujenzi wa vivuko vipya viwili vya MV. Ukara na MV. Chato vinavyojengwa na kampuni Songoro Marine ambavyo vipo katika hatua za mwisho za ukamilikaji. Ujenzi wa vivuko hivyo unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 8.2.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine, Mhandisi Major Songoro,  akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko vipya viwili vya MV. Ukara na MV. Chato, Mkoani Mwanza.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akiwa na Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mwanza, Bw. Salum Kali, wakielekea kukagua ujenzi wa vivuko vipya vya MV. Ukara na MV. Chato, mkoani Mwanza. Vivuko hivyo vinatarajia kuanza kutoa huduma mwezi Agosti, mwaka huu.

UKAMILISHAJI wa ujenzi wa Kivuko Kipya cha MV. Ukara kitakachotoa huduma kati ya Bugolora (Ukerewe) hadi Ukara (Ukara) kitakuwa mwarobaini kwa wakazi wa visiwa hivyo ambao mahitaji yao ya usafiri yamezidi kuongezeka.
Kivuko hicho ambacho kinajengwa na Kampuni ya Songoro Marine kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 300 pamoja na mzigo tani 100 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameyasema hayo akiwa mkoani Mwanza, wakati wa ziara yake mkoani hapo ambapo alikagua hatua zilizofikiwa za ujenzi wa kivuko hicho ambacho kinagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 4.7 na kuridhishwa na maendeleo yake.
"Watanzania nyinyi wenyewe mnajionea juzi tumepeleka Meli Bukoba lakini Serikali haiishi hapo tu inaendelea na ujenzi wa kivuko hiki ambacho kitasaidia katika kutoa huduma kwa wananchi wa visiwa vya ukara na ukerewe kwani mahitaji ya usafiri kati ya visiwa hivyo ni makubwa zaidi", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha, amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anafunga haraka vifaa ambavyo waliviagiza ili mapema zaidi ya mwezi wa nane  kivuko hicho kiwe majini na kianze kutoa huduma.
Kwandikwa, amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kubuni vivuko vipya vitakavyoweza kukidhi mahitaji ya ongezeko la watu kwa siku za usoni na miaka ijayo ambayo itasaidia kutatua changamoto za usafiri wa visiwani.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amekagua pia ujenzi wa kivuko kingine cha MV. Chato ambacho kinarajiwa kutoa huduma kati ya Chato hadi Nkome, mkoani Geita na kumsisitiza mkandarasi kukamilisha haraka kazi zilizobakia katika kivuko hicho ili nacho kianze kazi mapema mwezi Agosti mwaka huu.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa vivuko vipya, Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Hassan Karonda, amesema kuwa mpaka sasa ujenzi wa kivuko cha MV. Ukara umefikia asilimia 85 na MV. Chato asilimia 80 na miradi hii yote ikikamilika wataweza kuwahudumia wananchi wengi na kwa karibu zaidi.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine, Mhandisi Major Songoro amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa kazi ya kufunga vyuma imeshakamilika kwa vivuko vyote kwa asilimia 95, tayari injini zimeshafungwa na kazi zilizobakia ni za kuweka milango, madirisha, viti, mifumo ya umeme na kupaka rangi.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Mwanza, Bw. Salum Kali, ameishukuru Serikali kwa hatua ya ujenzi wa vivuko hivyo ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo imelenga kusaidia kuondoa adha ya usafiri kwa wananchi wanaoishi katika visiwa hivyo.

No comments:

Post a Comment