Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. |
RAIS wa Kenya Uhuru Kenyatta ameondoa masharti ya usafiri wa kuingia na kutoka katika miji ya Nairobi, Mombasa na Mandera kaskazini mwa nchi. Katika hotuba yake kwa taifa kuhusu mwenendo wa maambukizi ya virusi vya corona rais Kenyatta amesema hatua ya kufungua miji hiyo mitatu ''inawaweka Wakenya'' katika hali hatari na hivyo basi naomba tuwe waangalifu.
Bw. Kenyatta hata hivyo ametangaza kuwa muda wa kutotoka nje usiku kati ya saa saa tatu usiku hadi saa kumi alfajiri umeongezwa kwa siku thalathini.
''Lazima tutambue tuko katika hatari zaidi ya vile tulivyokuwa wakati kuna masharti, tutachunguza mienendo ya watu, na kama hali itakuwa mbaya tena tutarejea katika lockdown'' Alisema Rais Kenyata.
Rais Kenyatta pia ametangaza kufunguliwa kwa maeneo ya kuabudu kwa awamu kwa kuzingatia muongozo wa kuzuia maambukizi ya corona uliowekwa na wizara ya Afya.
''Tusidanganyane kwamba ugonjwa haupo sana, twasikia watu wakisema huu ugonjwa sio wa kweli kwasababu hakuna mtu anayemjua mtu aliyeambukizwa'' alisema rais Kenyatta.
Wakati huo huo Bw. Kenyatta amewasihi viongozi wote wakiwamo wa kidini kuchukuwa jukumu la kuzuia kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa corona.
Maeneo ya kuabudu yametakiwa kuwa na waumini wasiozidi 100 katika kila ibada itakayofanyika na ibada zitafanyika si zaidi ya kipindi cha saa moja.
Makanisa yakitarajiwa kufunguliwa baada ya wiki tatu baada kufanya mashauriano baina ya viongozi wa kidini.
Mafunzo ya shule ya Jumapili na Madrassa yataendelea kufungwa mpaka maelekezo mengine yatakapotolewa.
Rais Kenyatta ametangaza kuwa safari za ndege ndani ya Kenya zitaanza tena tarehe 15 mwezi Julai mwaka 2020; kwa kuzingatia miongozo na kanuni kutoka kwa wataalamu wa afya kutoka wizara ya afya na mamlaka ya usafi wa anga nchini humo.
Safari za kimataifa za kuingia na kutoka nchini zitaanza tarehe 1 mwezi Agosti 2020.
-BBC
No comments:
Post a Comment