DKT CHAULA AHAIDI MABADILIKO SEKTA YA MAWASILIANO, ASISITIZA UWAJIBIKAJI NA MAHUSIANO BORA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 15 June 2020

DKT CHAULA AHAIDI MABADILIKO SEKTA YA MAWASILIANO, ASISITIZA UWAJIBIKAJI NA MAHUSIANO BORA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Zainabu Chaula akizungumza na wafanyakazi wa Sekta yake katika kikao cha wafanyakazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa TBA, Dodoma. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Jim Yonazi na kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utumishi na Rasilimali Watu, Kitolina Kippa.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainabu Chaula ameahidi kuleta mabadiliko chanya katika Sekta ya Mawasiliano  na kuwataka watumishi wa Sekta hiyo kuuvua unyonge na kufanya kazi kwa kufuata miongozo na kushirikiana katika kutekeleza wajibu na majukumu yao kwa bidii, weledi na uzalendo. 

Dkt. Chaula ameyasema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao chake na watumishi wa Sekta hiyo alichokifanya kwa mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuongoza Sekta hiyo tarehe 22 mwezi Aprili mwaka huu ambapo  kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Majengo (TBA), Dodoma

Katika kikao hicho, Dkt. Chaula ametoa rai kwa watumishi wa Sekta ya Mawasiliano kuboresha mahusiano yao mahali pa kazi ikiwa ni pamoja na kupeana taarifa sahihi na kwa wakati ili watumishi wote wawe na uelewa wa pamoja kuhusu majukumu na miradi inayotekelezwa na Sekta hiyo.

Pia, amesisitiza kuboresha mahusiano mazuri kati ya Sekta na taasisi zake ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Tume ya TEHAMA (ICT Commisison) ili kuwa na ushirikiano na kujenga uelewa wa pamoja katika kutekeleza majukumu ya Serikali ya kuhudumia wananchi.

“Mahusiano yetu tunayajenga sisi wenyewe, iwe ni mahusiano ya ndani ya Sekta au kati ya Sekta na taasisi inazozisimamia, ninataka kila mtu awajibike katika nafasi yake ili mwishoni aweze kusema ameifanyia nini Sekta ya Mawasiliano kwa kuwa mahusiano mazuri mahali pa kazi ni tunu ya utendaji mzuri wa majukumu kazini,” amesisitiza Dkt. Chaula

Pia, amewaasa watumishi wa Sekta hiyo kuwa watu wa kujifunza  na kukubali mabadiliko, kwasababu kila kitu kinatengenezwa kwa misingi mahususi  na kila kitu kinachofanywa na Serikali  ni kwa manufaa ya umma

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Dkt. Jim Yonazi amesisitiza watumishi kupendana na kushirikiana ili kufanya kazi katika mazingira rafiki na yenye utashi zaidi.

Ameongeza kuwa milango ya ofisi yake na ya Dkt. Chaula ipo wazi kusikiliza na kushughulikia kero na matatizo ya watumishi na kuwaasa watumishi wasikae na kero zao moyoni.

Naye mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Mawasiliano, Bi. Laurencia Masigo amempongeza Dkt. Chaula kwa kurejesha imani na matumaini kwa wafanyakazi wa Sekta hiyo kwa kipindi kifupi tangu ameteuliwa kuongoza Sekta hiyo na kuahidi kuwa wafanyakazi hawatamuangusha na wako tayari kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Mawasiliano inaendelea kukua, kuchangia pato la taifa na kuhudumia wananchi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment