Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe |
Na Shamimu Nyaki – WHUSM
WIZARA YA HABARI, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaratibu ujenzi wa Sanamu ya Mwalimu Julius Kamabarage Nyerere katika viwanja vya jengo la Amani na Ulinzi la Julius Nyerere lililopo katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) Jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa Hutoba ya Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2020/2021 Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa ujenzi wa sanamu hiyo ni utekelezaji wa Azimio la Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Jijini Harare, Zimbabwe mwaka 2015.
“Ujenzi wa Sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere katika Umoja wa Afrika (AU) ni makubaliano ya mkutano wa wakuu wa nchi wa SADC ambao walikuabaliana kuwa ujenzi huo lengo lake ni kutambua na kuenzi mchango wa waanzilishi wa SADC katika kulikomboa Bara la Afrika” alisema Dkt. Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa ujenzi wa Sanamu hiyo utatumia malighafi ya Shaba nyeusi (bronze statue) ambapo ameeleza kuwa Kamati ya Kitaifa ya Uratibu na Kamati ya Ujenzi wa Sanamu za Kuwaenzi Waasisi wa Taifa kama inavyotakiwa katika sheria ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa ya mwaka 2004 zimeshaundwa na kuanza kazi tangu 2018.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa mradi huo Dkt. Emmanuel Ishengoma ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa katika Wizara ya Habari, Utaaduni, Sanaa na Michezo amesema kuwa hatua za awali za ujenzi wa Sanamu hiyo tayari zimeanza na mradi unatekelezwa na Kampuni ya SAMCRO ya nchini Afrika Kusini chini ya usimamizi wa SADC na Tanzania na utagharimu takriban Dola za Marekani 267,992.60 ambazo ni sawa na takriban Shilingi 615,000,000 ambazo zitatolewa na SADC na gharama za usimamizi kutolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Ishengoma ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu ambapo Sehemu kubwa ya kazi hiyo itafanyika nchini Afrika Kusini na ikiishakamilika na kuridhiwa na Tanzania pamoja na SADC itasafirishwa na kusimikwa katika Makao Makuu ya AU huko Addis Ababa Ethiopia.
Ujenzi wa Sanamu hiyo umetokana na wazo alilolitoa Rais wa zamani wa Zimbabwe Hayati Robert Mugabe katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kuhusu mkakati wa kuwaenzi viongozi waanzilishi wa SADC ambao walishiriki katika kulikomboa Bara la Afrika.
No comments:
Post a Comment