Wadau mbalimbali wakishiriki uzinduzi wa Mradi mpya wa taasisi ya Save The Children ambapo mradi huo mpya utajikita katika kuongeza ushiriki wa wananchi katika michakato ya kisera na Kibajeti. |
MKUU wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amewataka wadau kwa kushirikiana na serikali waendelee kutoa msaada kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwani bado wengi hawajafikiwa.
Brig. Jen. Mwangela ameyasema hayo wakati akishiriki uzinduzi wa Mradi mpya wa taasisi ya Save The Children ambapo mradi huo mpya utajikita katika kuongeza ushiriki wa wananchi katika michakato ya kisera na Kibajeti.
Amesema taasisi hiyo imekuwa ikisaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hivyo miradi mingine watakayo ianzisha wasisahau lengo kuu la taasisi hilo la kusaidia watoto kwakuwa bado wapo wengi wenye matatizo ambao bado hawajafikiwa.
Brig. Jen. Mwangela amesema wadau hao wa Save the Children pamoja na wengine wanaendelea kualikwa kuwasaidia watoto walioko katika mazingira hatarishi pia kutoa elimu kwa jamii kwakuwa bado elimu ya kupambana na ukatili wa watoto bado haijafika kote.
Ameongeza kuwa mradi huo mpya ulioanzishwa ni mzuri na tayari serikali imesha fanya kwa hatua kubwa hasa kwa kuboresha huduma za kijamii kama elimu, maji na afya pamoja na kutoa uwazi kwa wananchi kushiriki katika huduma hizo hivyo wadau wanapaswa kusaidiana na serikali katika jitihada ambazo tayari zimeanzishwa.
Meneja Mradi wa kuongeza ushiriki wa wananchi katika michakato ya kisera na kibajeti kwa Mkoa wa Songwe John Tobongo amesema mradi huo unatarajia kufanyika katika Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe, Shinyanga na Zanzibar na utagharimu Euro laki tano.
Tobongo amesema matarajio ya mradi huo ni kuwafikia wananchi wa Mbozi 524,450 huku ukijumuisha na watoto pia utatekelezwa kwa mwaka 2020 hadi 2021.
No comments:
Post a Comment