WIZARA YA AFYA YATOA UFAFANUZI MASWALI YA WANANCHI KUHUSU CORONA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 2 April 2020

WIZARA YA AFYA YATOA UFAFANUZI MASWALI YA WANANCHI KUHUSU CORONA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akionyesha umbali ambao mtu anapaswa kukaa ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Na WAMJW, Dar es Salaam


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema amekuwa akipokea maoni, maswali na ushauri kutoka kwa wananchi wakitaka kujua jitihada mbalimbali za Serikali za kukabiliana na homa kali ya mapafu na amewaagiza wataalamu wake kuanza  kujibu maswali.

Waziri Ummy amesema maswali, maoni na ushauri huo unatoka kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na kituo cha wizara cha kupokea simu kuhusu ugonjwa wa homa ya Corona.

“Moja ya swali linaloulizwa kutoka kwa wananchi ni suala la kupima ugonjwa wa Corona (covid-19), hivyo katika kutoa ufafanuzi ni vema  Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dkt. Nyambura Muremi, aeleze Watanzania nani anakidhi vigezo vya kupima ugonjwa wa Covid-19 na taratibu za kupima ugonjwa huu zikoje,” amesema Ummy Mwalimu.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy Mwalimu amesisitiza wananchi kwamba wanapaswa kukaa umbali wa mita mbili kati ya mtu mmoja na mtu mwingine ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Akizungumzia kuhusu maswali ya wananchi, Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Dkt. Nyambura Muremi amesema kuwa anayepaswa kupimwa ugonjwa wa corona ni yule aliyetimiza vigezo kama vile mtu kuwa na dalili ya ugonjwa wa covid-19.

“Kama mtu amepata kirusi, ataanza kuonyesha dalili kama vile kupata homa, hapa ndio tutanza kuchukua kipimo na huu ndio uthibitisho wa kisayansi,” amesema Dkt. Muremi.

Akizungumzia taratibu za kupima ugonjwa wa corona, Dkt. Muremi amesema katika ngazi ya mkoa wapo wataalamu wanashughulika kupima sampuli na kwamba wao ndio wamekuwa wakiratibu  shughuli zote za kimaabara kila mkoa.

“Baada ya kupima huko mikoani wanaleta Maabara Taifa ya Afya ya Jamii ambayo ina vigezo vitatu vinavyotambulika kimataifa,” amefafanua Dkt. Muremi.

Dkt. Muremi ametaja vigezo vya Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ni kwamba ina usalama wa kibailojia ngazi ya tatu (BSL-3), wataalamu waliothibitishwa kupima magonjwa hatarishi na mashine stahiki ambayo imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kutokana na maswali mengi ya Wananchi kuanzia sasa Wizara ya Afya itaendelea kujibu maswali yao.

No comments:

Post a Comment