WABUNGE UNGENI MKONO MABORESHO SHERIA YA USALAMA BARABARANI, ROHO ZINATEKETEA...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 15 April 2020

WABUNGE UNGENI MKONO MABORESHO SHERIA YA USALAMA BARABARANI, ROHO ZINATEKETEA...!

Spika wa Bunge la Tanzania, Bw. Job Yustino Ndugai akiendesha moja ya vikao vya bunge.

Na Joachim Mushi, Dar

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaendelea na Mkutano wa 19 wa Bunge, ambao kipindi hiki unafanyika kwa tahadhari kubwa kukabiliana na ugonjwa wa Corona unaosababishwa na virusi vya COVID 19. Miongoni mwa kazi zitakazofanywa na mkutano huu ni pamoja na kupitisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021, kutunga Sheria kwa kupitisha Miswada ya Sheria pamoja na Hoja mbalimbali.

Nchini Tanzania 'mdudu' ajali za barabarabi amekuwa akipoteza maisha ya Watanzania wengi na huku akiacha vilema wa kudumu na wategemezi wengi ambao ni mzigo kwa taifa pia. Kama hiyo haitoshi, nguvu kazi ya taifa, mali za watu pamoja na miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa imekuwa ikiharibiwa na ajali hizi.

Hata hivyo, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2018 zinaonesha zinabainisha takribani watu milioni 1.35 hufariki kila mwaka kutokana na ajali za barabarani. Janga hili la ajali za barabarani hugharimu nchi husika karibu asilimia tatu ya pato la taifa, huku asilimia 93 ya ajali hizo zikionesha kutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati ikiwemo Tanzania.

Mfano takwimu za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani za mwaka 2016 kuanzia mwezi Agosti hadi Novemba zinaonesha kulikuwa na jumla ya ajali 785 zilizosababisha vifo vya watu 298 ndani ya takribani miezi minne tu. Na takwimu za mwaka 2017 za ajali za barabarani za kikosi hicho kuanzia Mwezi Januari hadi Septemba zilisababisha jumla ya vifo 1906.

Takwimu pia zinaonesha kuwa ajali nyingi zinatokea kwa sababu ya makosa ya kibinadamu hasa uzembe wa madereva kutokutii sheria na kanuni za barabarani, ambapo kwa mujibu wa taarifa za jeshi la polisi nchini Tanzania, asilimia 76 ya ajali barabarani husababishwa na uzembe wa madereva, asilimia 8 husababishwa na ubovu wa barabara, na huku hali ya ubovu wa vyombo vya moto kusababisha ajali kwa asilimia 16.

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) inasema njia kuu ya usafiri ya barabara licha ya kuchukua asilimia 90 ya abiria na robo tatu ya mizigo, ndio inayoongoza kutoaminika kiusalama ajali zake zinachangia sana wastani wa vifo vya watu 4,000 kwa mwaka.

Baadhi ya ajali zinazotokea na kugharimu maisha ya watu, nguvu kazi ya taifa na mali.

Maadhirimisho ya tano ya Wiki ya Umoja wa Mataifa ya Usalama Barabarani kwa Mwaka 2019, yalifanyika kwa wadau wanaoshinikiza maboresho ya sheria ya usalama barabarani wakiwemo; TAMWA, TAWLA, GHAI, TMF, SHIVYAWATA, SIKIKA, TLS pamoja na RSA kupaza sauti kwa vyombo husika kuridhia maboresho ya Sheria ya Usalama Barabarani nchini Tanzania ya mwaka 1973.

Kimsingi Sheria hii licha ya kuendelea kufanyiwa maboresho kipindi hadi kipindi bado inamapungufu. Hadi kufikia mwaka 2018 marekebisho makubwa ya sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 yaliyofanywa ni yale ya mwaka 1996. Maeneo ambayo yanapendekezwa na asasi hizo na nyinginezo zinazopambana na ajali hizo ni pamoja na; Matumizi ya mikanda ambapo Sheria inasema ni kosa kisheria kwa dereva na abiria anayekaa kiti cha mbele kutokufunga mkanda kwenye safari lakini sheria ipo kimya juu ya abiria wanaokaa viti vya nyuma.

Sheria ya sasa pia inaeleza ni kosa kwa muendesha pikipiki kutokuvaa kofia ngumu wakati wa kuendesha chombo hicho, Lakini sheria haisemii chochote kwa abiria wa chombo hicho. Vilevile sheria haielezi ni jinsi gani kofia inatakiwa kuvaliwa na aina maalum ya kofia inayotakiwa kuvaliwa. Kwa mujibu wa Utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonyesha kuwa iwapo ajali itatokea madhara yanayotokea kwa kutovaa kofia maalum na kwa usahihi ni makubwa sana ukilinganisha na kofia hiyo ikivaliwa na kwa usahihi.

Ieleweke kuwa Sheria ya sasa ya usalama barabarani inasema ni kosa mtu yoyote kuendesha chombo cha moto akiwa na kiwango cha kilevi katika damu yake kinachozidi asilimia 0.08% katika mfumo wa mwili. Kiwango hiki ni kikubwa sana kikilinganishwa na tafiti zilizofanywa na Shirika la afya duniani na kupendekeza kiwango asilimia 0.05% kwa dereva aliyebobea (experienced driver) na asilimia 0.02% kwa dereva mchanga (young driver).

Baadhi ya ajali zinazotokea na kugharimu maisha ya watu, nguvu kazi ya taifa na mali.
Eneo la mwendo kasi pia limeendelea kuwa sababu kubwa ya ajali zinazogharimu uhai wa watu wengi. Sheria yetu inayo mapungufu kadhaa pamoja na juhudi nyingi za Jeshi la Polisi na wadau wengine kutaka kudhibiti jambo hili lemeendelea kuwa tatizo. Adhabu zisiszokidhi wala kuleta hofu kwa maderava wasiotaka kutii zimeendelea kufifisha juhudi za kudhibiti tatizo hili.

Pamoja na mambo mengine wabunge ambao ni wawakilishi wetu katika mkutano wa 19 unaoendelea jijini Dodoma wanaweza kulibeba hili na kuungana asasi hizi na jamii kupigania maboresho ya sheria hizi ambazo bado zinatoa mwanya kwa waendeshaji vyombo hivyo kutozingatia sheria kutokana na mianya iliopo kwa sasa. Muhimili huu endapo ukiguswa na kulibeba ni rahisi kuchochea maboresho hayo.

No comments:

Post a Comment