SINGIDA YAWA MWENYEJI KITAIFA UZINDUZI RASMI WA PROGRAMU YA MAPAMBANO DHIDI YA KUENEA KWA VIRUSI VYA CORONA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 3 April 2020

SINGIDA YAWA MWENYEJI KITAIFA UZINDUZI RASMI WA PROGRAMU YA MAPAMBANO DHIDI YA KUENEA KWA VIRUSI VYA CORONA

 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana  Wasomi kutoka katika kada tofauti nchini (TYEC) Ojung Ole Saitabau akizungumza wakati  wa uzinduzi rasmi wa Programu ya mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa corona mkoani Singida jana.  

 Baadhi ya Vijana kutoka TYEC wanaojitolea  kutoa elimu  ya mapambano dhidi ya kuenea kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona wakiwa kwenye uzinduzi huo.

 Afisa Afya  kutoka Manispaa ya Singida, aliye mwakilisha mganga mkuu wa mkoa huo, Roman Anselimi (katikati) akizindua kampeni hiyo. Kutoka kulia ni  Mwenyekiti wa TYEC, Ojung Ole Saitabau na Afisa Afya  kutoka Manispaa ya Singida, Aneth Kanywa.

 Afisa Afya  kutoka Manispaa ya Singida, Aneth Kanywa, akizungumza.

TYEC wakianza rasmi safari ya utekelezaji wa kampeni dhidi ya mlipuko wa corona.

Mratibu wa Kamati ya Programu ya mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa corona kutoka TYEC Mkoa wa Singida, Stella Mwagowa pamoja na Mratibu wa Uhamasishaji na Utoaji wa Elimu ya Afya Mkoa wa Singida, Paul Sangalali wakitoa elimu ya namna ya kujikinga na Virusi vya Corona kwa mmoja wa wafanyabiashara.

 Afisa wa Polisi, Rashid Mirambo akitoa elimu ya namna ya kujikinga na Virusi vya Corona kwa vijana.

 Mmoja wa Wanajumuiya ya TYEC, Richard Assey, akishiriki kampeni hiyo kwa kutoa elimu dhidi ya mlipuko wa virusi vya corona kwa mmoja wa wafanyabiashara wa chakula.

 Maelekezo ya namna ya kusafisha mikono kwa usahihi ni mojawapo ya shabaha ya kampeni hiyo.

 Kampeni ikiendelea.

 Kampeni ikiendelea kwa wauza nyama.

Kampeni ikiendelea.

Na Mwandishi Wetu, Singida

TIMU ya vijana wa kitanzania ambao ni wasomi na wabobevu kutoka katika kada tofauti (TYEC) hatimaye wamefanya uzinduzi rasmi  wa Programu ya mapambano dhidi ya kuenea kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona.

Hafla ya uzinduzi huo kitaifa umefanyika mkoani hapa, sambamba na timu hiyo kuanza kutekeleza kampeni hiyo kwa kutembelea maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko na kutoa elimu ya kinga dhidi ya ugonjwa huo hatari kama sehemu ya kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na serikali.

Endapo watapata vibali kutoka kwenye mamlaka husika staratejia waliyonayo ni kuhakikisha wanatumia kila aina ya vipawa, elimu na uwezo walionao katika kufikia na kutoa elimu kwa mtu mmoja-mmoja, makundi na taasisi nyingi iwezekanavyo kuhusiana na janga hilo linaloendelea kutikisa kwa sasa duniani kote.

Baadhi ya maeneo waliyotembelea sambamba na kupata fursa ya kutoa elimu mkoani hapa jana ni pamoja na eneo la Soko Kuu la Manispaa ya Singida, vituo vya bajaji-ambapo ziara hiyo iliwakutanisha na kuzungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa aina tofauti na madereva wanaoendesha bajaji.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo,  Mwenyekiti wa TYEC Taifa, Ojung' Ole Saitabau alisema kila mtanzania anapaswa kuchukua tahadhari na kamwe asipuuze ushauri wa kitaalamu unaoendelea kutolewa na serikali ili kwa pamoja tuweze kuishinda vita dhidi ya corona.
Saitabau   alisema homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona ni ugonjwa unaoambukizwa kwa kuingiwa na majimaji yatokayo kwenye njia ya hewa wakati mtu mwenye ugonjwa huo anapokohoa au kupiga chafya.

Hata hivyo akizungumza kwa niaba ya mganga mkuu wa mkoa wa Singida, Afisa Afya kutoka Manispaa ya mkoa huo, Roman Anselimi alisema njia nyingine ya maambukizi ni kwa kugusa majimaji yanayotoka puani (kamasi), kugusa vitambaa au nguo zilizotumiwa na mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huo, au maeneo mengine yaliyoguswa na mtu mwenye Virus vya ugonjwa huo.

“Ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba ya moja kwa moja  hivyo kama yalivyo magonjwa yanayosababishwa na virusi, matibabu hufanyika kwa kuzingatia dalili zilizopo na ufuatiliaji wa karibu,” alisema Anselimi.

 Akielezea jinsi ya kujikinga na homa ya Virusi vya corona Afisa mwingine wa Afya kutoka Manispaa ya Singida, Aneth Kanywa alitoa tahadhari ya watu kukaa mbali angalau mita 1 au 2 na mtu mwenye dalili za homa au kikohozi mwenye historia ya kusafiri maeneo yenye mlipuko wa ugonjwa huo.

Tahadhari nyingine ni pamoja na kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kutumia kitambaa safi au sehemu ya mbele ya kiwiko cha mkono, epuka kugusana na mgonjwa mwenye dalili za homa na kikohozi, kusalimiana kwa kushikana mikono, kukumbatiana au kubusiana.

Tahadhari nyingine ya jinsi ya kujikinga pamoja na mambo mengine ni kuepuka kugusa macho, pua au mdomo, subiri au epuka safari zisizo za lazima kwenda kwenye maeneo yalioathirika na inapolazimu kusafiri pata maelezo ya kitaalamu kabla ya kuondoka nchini na epuka misongamano.

"Safisha mikono yako mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kwa dawa ya kutakasa mikono, ukiona mojawapo ya dalili za ugonjwa huu, wahi kituo cha huduma za afya, vilevile toa taarifa kwenye kituo cha huduma za afya uonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa huo," alisema Kanywa.

Hata hivyo kwa mujibu wa Mratibu wa kamati ya kampeni hiyo, Stella Mwagowa alisema utekelezaji wa programu hiyo unatarajia kuwafikia wananchi wa wilaya zote mkoani hapa, huku shughuli nyingine za kitaifa  zikiendelea kuratibiwa na TYEC kwenye mikoa mingine.

No comments:

Post a Comment