KINONDONI YAPULIZA DAWA HOTELI ZA KITALII KUDHIBITI CORONA KWA KUTUMIA MAGARI YA ZIMAMOTO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 3 April 2020

KINONDONI YAPULIZA DAWA HOTELI ZA KITALII KUDHIBITI CORONA KWA KUTUMIA MAGARI YA ZIMAMOTO

Kaimu Mganga mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Dk. Abduli Hemed mwenyekoti la bluu akihakiki gari la zimamoto kabla ya kuanza kwa zoezi la umwagiliaji dawa katika hotel zakitalii eneo la Masaki.

Mmoja wa maafisa wa zimamoto akipulizia dawa kwenye maeneo mbalimbali ya hoteli za kitalii zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.


HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imeendelea kupambana vikali kuthibiti kuenea kwa virusi vya COVID 19 (Corona) kwa kupuliza dawa katika hotel za kitalii zilizopo katika Halmashauri hiyo.

Hatua hiyo ni muendelezo wa mkakati uliowekwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Daniel Chongolo, Mkurugenzi Aron Kagurumjuli, Mstahiki Meya Benjamini Sitta, pamoja na Mganga mkuu Samweli Laizar kwa pamoja, katika kuhakikisha kuwa  maambukizi ya  Virus hivyo hayasambai kwa wananchi na hivyo wanaendelea kuwa salama.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo Kaimu Mganga mkuu wa Kinondoni, Dk. Said Hemed amesema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa salama katika kuepukana na maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.

Amefafanua kuwa mbali na kuthibiti maambukizi ya virusi vya Corona, lakini pia wanachukua tahadhari ya mlipuko wa homa ya dengu kwakuwa hivi sasa ni kipindi cha mvua.

Ameongeza kuwa kupuliza dawa katika maeneo hayo ni mahususi kwakuwa wageni wengi hufikia katika hoteli hizo na kwamba wataendelea kuthibiti kwenye maeneo mbalimbali  ili virusi hivyo visienee kwenye makazi ya wananchi.

“ Tunapopuliza hizi dawa ni kwa malengo mawili, kwanza tunathibiti Corona isisambae lakini pia tunathibiti homa ya dengue, ukiangalia kipindi hiki ni cha msimu wa mvua, magonjwa mengi ya mlipuko hutokea , kwa hiyo hii ni njia ya kuwakinga wananchi wetu wa Kinondoni wasipate maambukizi yoyote” amesema Dokta Hemed.

Aidha ameongeza kuwa” hotel hizi za kitalii ni maarufu na ndio ambazo zinapokea wageni wengi, niwasishi sana waendelee kuchukua tahadhari kwakutoa ushirikiano na Halmashauri yetu ili mlipuko huu usiendelee kwenye maeneo watu.

Awali Kinondoni ilianza mchakato huo wa kupuliza dawa katika vituo vya daladala, mwendokasi, na maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo Kanisani na Misikitini pamoja na maeneo ya wananchi na kwamba bado zoezi hilo linaendelea.

Hadi sasa zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wa Kinondoni linaendelea kwani Kata 20 zilizopo kwenye Halmashauri zimeshafikiwa sambamba na matangazo ikiwemo kubandika mabango, kugawa vipeperushi kwa wananchi vyenye ujumbe wa kuelimisha namna ya kujikinga na virusi vya COVID19 ( Corona).

Imeandaliwa na Kitengo Cha Habari na Uhusiano

Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

No comments:

Post a Comment