BODI YA MAJI BONDE LA KATI YAWATAKA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 3 April 2020

BODI YA MAJI BONDE LA KATI YAWATAKA WANANCHI KUCHUKUA TAHADHARI...!

 Mhandisi Rasilimali za Maji, Bodi ya Maji Bonde la Kati, Moses Salumbi (kushoto),  akiweka alama za ukomo wa maji ya mafuriko kwenye Maziwa ya Kindai na Munang mkoani Singida jana.Wengine kutoka kulia ni Mhandisi Ujenzi, Danford Samson, Mhandisi Mazingira, Nyagheri Mramba, Afisa wa Maji, Bodi ya Maji  Bonde la Kati, William Mabula na Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa ofisi hiyo, Nelea Bundala.

 Athari za mafuriko hayo.

 Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi,  Bodi ya Maji  Bonde la Kati, Nelea Bundala, akionesha athari za mafuriko hayo. Kushoto ni Mhandisi Mazingira, Nyagheri Mramba.

Baadhi ya viwanda na Maghala yakiwa yamezingirwa na mafuriko.
  Athari za mafuriko hayo.

  Athari za mafuriko hayo.

 Muonekano wa ziwa Singidani kwa sasa.

 Wananchi wakiangalia hali isiyo ya kawaida ya ujazo wa maji uliosababisha Maziwa ya Kindai na Munang kuungana.

 Afisa wa Maji, Bodi ya Maji  Bonde la Kati, William Mabula (kulia), akiongozana na maofisa wengine kwenda kuweka alama za ukomo wa maji ya mafuriko kwenye Maziwa ya Kindai, Munang na Singidani.

 Athari za mafuriko hayo.

 Mhandisi Mazingira kutoka Bodi ya Maji  Bonde la Kati, Nyagheri Mramba, akiweka alama za ukomo wa maji pembezoni mwa Ziwa Kindai.

 Baadhi ya Watendaji wa Sekta za Umma, Jeshi la Polisi na Maofisa wa Bodi ya Maji Bonde la Kati wakiwa  kwenye eneo hilo.    

 Mwenyekiti wa Mtaa wa Stesheni, Kata ta Utemini, Juma Kanka, akizungumzia mafuriko hayo.

Mhandisi Rasilimali za Maji, Bodi ya Maji Bonde la Kati, Moses Salumbi, akizungumzia zoezi la  uwekaji alama za ukomo wa maji kwenye maziwa hayo.

Na Waandishi Wetu, Singida

KUFUATIA mvua za masika zinazoendelea, Bodi ya Maji Bonde la Kati imewataka wananchi wote waishio kwenye maeneo ya  vyanzo vya maji kuchukua tahadhari na ikiwezekana kuondoka mara moja, ili kujiepusha na majanga yanayoweza kujitokeza zaidi kwa kipindi hiki ikiwemo vifo. Sambamba na hilo, bodi hiyo imeanza rasmi kuweka alama za ukomo wa maji ya mafuriko kwenye maziwa ya Kindai, Munang na Singidani ambazo zitasaidia kutambua hifadhi sahihi ya maziwa hayo. Kabla ya kuanza zoezi la kuongeza mita 60 ambazo zipo kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa maziwa nchini.

Akizungumza wakati akikagua athari za mafuriko yaliyotokana na kupitiliza kwa ujazo wa maji kwenye maziwa ya Kindai na Munang, Afisa wa Maji, Bodi ya Maji  Bonde la Kati, William Mabula aliwataka wananchi wote waishio kwenye maeneo hatarishi ya vyanzo vya maji kuchukua tahadhari.

“Mvua hizi ni kubwa na huenda zikaendelea kunyesha kwa kipindi kirefu, niwatake tu wananchi waliojenga na hata wengine wanaoendeleza shughuli za kibinadamu kwenye maeneo haya ya chanzo cha maji wachukue tahadhari mapema kabla hatari kubwa zaidi hazijajitokeza,” alisema Mabula.

Alisema endapo mvua hizo zitaendelea kunyesha kwa kasi hiyo kulingana na utabiri unaotolewa na TMA, basi ni dhahiri maji nayo kupitia vyanzo na mikondo yake ya asili pia yataongezeka.

Akizungumzia kuhusu zoezi la uwekaji wa alama kwenye maziwa ya Kindai, Munang na Singidani unaoendelea, Mabula alisema ofisi hiyo tayari imeanza kuweka alama za muda mfupi sehemu ambazo maji ya mafuriko yanaishia, na wataendelea kusogeza alama hizo endapo maji yataongezeka.

“Tunaweka alama hizi ili zitusaidie kujua ukomo wa vyanzo hivi na hatimaye kuvihifadhi kwa usahihi, lakini pia zoezi hili litatupa taswira chanya hapo baadaye wakati wa kuongeza zile mita sitini ambazo zipo kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa maziwa nchini,” alisema Mabula.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi wa ofisi hiyo, Nelea Bundala, alisisitiza kwamba kwa hali halisi ya mafuriko ilivyofikia kwa sasa suala la wananchi kuondoka kwenye maeneo ya vyanzo hivyo vya maji haikwepeki.

Alisema kwa mwaka huu mvua za masika zimekuwa juu ya wastani, na vyanzo vya maji karibu maeneo yote vimejaa, mathalani kwenye baadhi ya mabwawa na maziwa maji yameanza kupita kwenye utoro na yamekuwa ni mengi kuliko uwezo wa vyanzo vilivyopo.

“Niwaombe tu wananchi waanze kuchukua tahadhari ikiwezekana kuondoka maeneo haya kwa usalama wao…athari zake ni kubwa kama unavyotazama makazi ya watu yameendelea kuzama, shughuli za kibinadamu na miundombinu ya thamani kubwa vyote vimeathirika,” alisema Bundala na kuongeza:
“Tukiwa kama wasimamizi wa rasilimali za maji tunawasihi watu waepuke kuishi kwenye maeneo hatarishi yenye vyanzo vya maji, Kinachoonekana hapa sio kwamba maji yamevamia watu hapana! Haya maji yapo mahala pake pa asili na watu ndio wameyafata haya maji,” alisema Bundala.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Stesheni, Kata ya Utemini, Juma Kanka, alisema mtaa huo ambao upo jirani na maziwa mawili ya Kindai na Munang kwa sasa umeathirika kwa kiasi kikubwa ikiwemo viwanda na miundombinu kadhaa kufunikwa kwa maji  ikiwemo barabara ya magereza-Mwankoko.

“Kusema ukweli maji hayajawahi kuwa mengi kiasi hiki tulikuwa tukisikia tu historia za zamani…kinachotushangaza kwa sasa ni kwamba maji haya yanazidi kuongezeka wakati hakuna mvua sijui yanatoka wapi. Ila wakazi wameitikia wito wameanza kutoka taratibu,” alisema Kanka.

Zoezi la kuwela alama chini ya Bodi ya Maji Bonde la Kati ni mwendelezo baada ya jitihada kama hizo kufanyika kwenye maziwa ya Kisisi maarufu Murya, Masoweda, halmashauri ya Hanang-Basutu na sasa mkoani Singida kwenye maziwa ya Kindai, Munang na Singidani. 

No comments:

Post a Comment