WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanafunzi wanaosoma katika shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia wilayani Ruangwa wasome kwa bidii kwa sababu Serikali imewaboreshea mazingira na kuwaepusha na vishawishi.
“Mawazo na akili yenu yote iwe katika kusoma tu, tunataka kuona mkiendelea kusoma hadi kidato cha tano na sita ili ndoto zenu za kufika vyuo vikuu zitimie.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Machi 16, 2020) wakati akizungumza na walimu na wanafunzi alipotembelea na kukagua maendeleo ya shule hiyo ya wasichana iliyopo wilaya ya Ruangwa, Lindi.
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia ni ya bweni na ilibadilishwa kutoka shule ya msingi Mnacho ambayo ilianzishwa mwaka 1932 na Shirika la Wamisionari Wakatoliki chini ya Mwalimu Lucas Malia.
Waziri Mkuu ambaye alisoma katika shule msingi Mnacho kabla ya kubadilishwa, amesema mwaka 2017 alitembelea shule hiyo na kukuta majengo yamechakaa ndipo alipotafuta wadau na kuyafanyia ukarabati.
“Nilikuta hata jengo ambalo nilisomea lilikuwa limechakaa, tulitafuta fedha na kukarabati ikawa mpya. Tuliamua kufanya mabadiliko kwa kuzingatia watoto waliokuwa wakisoma hapa walikuwa wanatoka kijiji cha Ng’au na kipindi cha mvua walishindwa kuja shule kutokana na mto kujaa maji.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa baada ya kubadilisha shule hiyo na kuwa ya sekondari ya wasichana walijenga shule ya msingi katika kijiji cha Ng’au na kuwahamishia watoto waliokuwa wakisoma shule ya msingi Mnacho.
Amesema katika wilaya ya Ruangwa hakukuwa na shule ya sekondari ya wasichana, hivyo amefarijika sana kuona watoto wa kike wakianza kusoma kidato cha kwanza kwenye shule hiyo ya bweni.
Waziri Mkuu amesema lengo ni kuhakikisha shule hiyo inakuwa na kidato cha tano na sita kwa sababu ina vyumba vya madarasa na mabweni ya kutosha. “Kuwepo kwa kidato cha tano na sita kutawaongezea ari ya kusoma wanafunzi wengine.”
Kwa upande wao, wanafunzi wanaosoma kwenye shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia wameishukuru Serikali kwa kuanzisha shule hiyo kwakuwa imewaepusha na vishawishi.
Wakiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzao, Sharifa Mbunga, Irene Mkuti, Ikra Jirani na Mwanayazi Omary wamesema uwepo wa shule hiyo utaongeza ari ya kusoma kwa wanafunzi wa kike wilayani Ruangwa, hivyo wameahidi kusoma kwa bidii.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Gladness Makongwa amesema shule imedahili wanafunzi 75 wa kike waliopata ufaulu wa juu kutoka kata zote zilizo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.
No comments:
Post a Comment