SERIKALI imesema shule zote za awali, msingi na sekondari zitafungwa kwa siku 30 kuanzia leo Machi 17, 2020.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo (Jumanne, Machi 17, 2020) wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salam.
Amesema wanafuzi wa kidato cha sita walipaswa kuanza mitihani Mei 4, 2020 lakini nao pia watapaswa kusibiri Wizara ifanye utaratibu mwingine kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi.
Amesema mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima imesitishwa kuanzia sasa ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii.
Amezitaka wizara na taasisi zizitishe semina, warsha, makongamano na mikutano yote hapa nchini ambayo inahusisha washiriki toka nchi zenye maambukizi makubwa. “Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi makubwa, wanashauriwa wasitishe safari hizo,” amesisitiza.
Akielezea hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali ili kudhibiti ugonjwa huo, Waziri Mkuu amesema: “Serikali imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na aina nyngine. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iziandikie taasisi zake.”
Pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe maeneo yote yaliyobainishwa na kutengwa (vituo vya huduma na ufuatiliaji) kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa endapo watajitokeza katika maeneo yao yanakuwa na mahitaji yote muhimu na yanahudumiwa ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali tayari imetoa shilingi milioni 500 kati ya sh. bilioni moja zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizokuwa zianze Aprili 2, mwaka huu.
“Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizokuwa zianze Aprili 2, mwaka huu na kuagiza shilingi bilioni moja zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo, zipelekwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya maandalizi ya kujiweka tayari kudhubiti maambukizi ya CORONA. Serikali tayari imetoa shilingi milioni 500.”
Akielezea hatua zilizochukuliwa baada ya mgonjwa wa kwanza kubainika kuwepo nchini Tanzania, Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua hatua kwa kumchukua mgonjwa huyo na kumhifadhi kwenye eneo maalum kwa ajili ya kumpatia huduma (isolation).
“Pia, Serikali imefanya ufuatiliaji wa watu waliokutana na mgonjwa huyu tangu aingie nchini na kuwaweka kwenye karantini ya siku 14, na pia kuchukua sampuli kwa lengo la kubaini kama wameambukizwa virusi hivi,” amesema.
Ugonjwa huu umeingia nchini baada ya Mtanzania mwenye miaka 46 aliyesafiri kwenda nchi za Ubeligiji, Sweden na Denmark hivi karibuni, kupimwa na kuthibitika kuwa na virusi vya Corona (COVID-19).
Akielezea hatua zaidi zinazochukuliwa, Waziri Mkuu amesema licha ya hatua ambazo zimechukuliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Serikali itaimarisha ukaguzi na ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu ili kuwabaini wasafiri wenye dalili za ugonjwa na viashiria vyenye hatari.
“Tutaimarisha uwezo wa kupima sampuli kwa watu wanaohisiwa kuwa na viashiria au dalili za ugonjwa huu ambapo maabara yetu ya Taifa kwa sasa inao uwezo wa kutoa majibu kwa haraka.”
Amesema Serikali inaendelea kuwajengea uwezo (mafunzo) watumishi wa sekta ya afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo jinsi ya kutoa tiba, kuchukua sampuli, uelimishaji na kuzingatia kanuni za afya.
“Serikali imetenga hospitali maalum za Mloganzila (DSM), Kituo cha Buswelu (Mwanza) na Hospitali ya Mawenzi (Kilimanjaro), Mnazi Mmoja (Zanzibar) na ChakeChake (Pemba) kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika.”
Ameiagiza Wizara ya Afya ihakikishe vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kudhibiti maambukizi (hand sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida na kuongeza kwamba Serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya ulanguzi wa vifaa hivyo.
Amewataka Watanzania wazingatie ushauri unaotolewa na Serikali na kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii. “Watanzania tuache mzaha wa kutumia mitandao ya kijamii kufanya upotoshaji wa tahadhari katika jambo hili,” ameonya.
Amewaomba viongozi wa dini waendelee kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha waumini wao wote kuzingatia tahadhari za ugonjwa huu. Pia amevitaka vyombo vyote vya habari vishirikiane na Serikali katika utoaji wa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na Corona bila kufanya upotoshaji wala kuipa jamii hofu.
Amewataka wananchi watoe taarifa kuhusu uwepo wa mgonjwa au kupata ufafanuzi kuhusu ugonjwa huu kupitia namba za bure za 0800110124, 0800110125 na 0800110037.
No comments:
Post a Comment