KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imewahikikishia ajira wananchi wa maeneo ya Mbagala katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kwa awamu ya pili unaoendelea kutekelezwa jijini Dar es Salaam.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, wakati aliposimamishwa na wananchi wa maeneo hayo wakati kamati hiyo ilipokuwa ikikagua ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi Synohydro Corporation kutoka china kwa muda wa miezi 36.
Kufuatia maelezo ya wananchi hao, Mwenyekiti huyo ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanasikiliza kero za wananchi hao ili kuwe na usawa kwenye ajira ambazo zinatolewa kwa wazawa.
"Kilio chenu tumekipokea na sisi kama Kamati tunatoa agizo kwa msimamizi wa mradi kulisimamia hili kwa haki na usawa kwani huu mradi ni wa kitaifa na ndo umeanza", amesisitiza Kakoso.
Ametoa wito kwa wananchi waliopo maeneo jirani na miradi yote inayoendelea kutekelezwa nchini kulinda na kuthamini miradi hiyo kwa kutojihusisha na vitendo vya uhujumu wa miunbombinu kwa kuiba mafuta na vifaa vya ujenzi.
"Watanzania mkipewa kazi kwenye miradi itunzeni iyo heshima mliyopewa kwa kutoshiriki katika matukio ya wizi wa mafuta, saruji na vitu vingine visivyopendeza", amesema Kakoso.
Kuhusu suala la utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa awamu ya pili ya miundombinu ya BRT, Kamati imeipongeza Serikali kwa hatua iliyofikiwa na wataalamu wa ujenzi wa miundombinu hiyo yenye lengo la kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Ameitaka TANROADS kumsimamia mkandarasi vizuri ili aweze kukamilisha miundombinu hiyo kwa muda uliopangwa.
"Tunajua kuwa kila siku idadi ya watu inaongezeka hivyo tunahitaji miundombinu imara ambayo iko salama ili itufikishe kwenye uchumi wa kati", amesema Mwenyekiti huyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Mchafu, ameishauri TANROADS kutoelekeza mifereji ya maji katika makazi ya watu ili kunusuru uhabirifu wa mazingira na mali zao.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Zuberi Kuchaukwa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Liwale, amewataka wataalamu wa usanifu wa miradi ya barabara nchini kutumia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kupanga vizuri namna ya kuboresha miundombinu hiyo kwa kuwa na madaraja makubwa na makalvati sehemu husika.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameihakikishia kamati hiyo kutekeleza maelekezo yote yaliyoelekezwa kwa Wizara na TANROADS na kuusimamia mradi wa BRT kwa viwango na ubora.
Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Crispianus Ako, ameieleza kamati hiyo kuwa ujenzi wa mradi huo unahusisha barabara yenye urefu wa kilometa 20.3, Flyovers mbili (2), vituo vya mabasi 29, daraja moja la waenda kwa miguu, ujenzi wa karakana (Depot) 1, vituo vikuu vya mabasi (Terminals) 2 na vituo mlisho viwili (2).
Ujenzi wa Miundombinu ya usafiri wa haraka wa mabasi (BRT), awamu ya pili unahusisha barabara ya Kilwa (Kamata hadi Mbagala), barabara ya Chang'ombe/Kawawa (Magomeni hadi Mgulani) na barabara ya Sokoine (Gerezani - City Hall).
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment