SERIKALI YAJIVUNIA VIWANGO VYA UTABIRI WA TMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday 25 March 2020

SERIKALI YAJIVUNIA VIWANGO VYA UTABIRI WA TMA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe akizungumza.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KILA ifikapo tarehe 23 Machi, ya kila mwaka Jumuiya ya kimataifa ya hali ya hewa duniani kote inaadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Siku hii ni kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), lililoanzishwa mwezi Machi 23, 1950.

Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa WMO, mbayo imeendelea kutekeleza maridhiano ya kimataifa katika sekta ya hali ya hewa kwa kuhakikisha Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) inatoa huduma za hali ya hewa katika viwango vinavyokubalika kimataifa.

Utekelezaji huo ni pamoja na kuijengea uwezo Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa upande wa vifaa na wataalam ili kuhakikisha wanafuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazohitajika nchini, kikanda na kimataifa kwa matumizi ya sekta zote ikiwa ni pamoja na sekta ya maji.

Mwaka jana, 2019, Serikali ilipitisha sheria ya kuhuisha Wakala wa Hali ya Hewa nchini kuwa Mamlaka kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya 2019. Sheria hii inaiwezesha Mamlaka kutekeleza majukumu yake kitaifa, kikanda na kimataifa na kutoa huduma za hali ya hewa kwa jamii ambazo zina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Sheria iliyounda Mamlaka ya Hali ya Hewa inaipa nguvu za kisheria za kudhibiti huduma za hali ya hewa hapa nchini na kukusanya mapato yanayotokana na matumizi ya huduma za hali ya hewa zinazotumiwa kibiashara. Pi sheria hiyo inaitambua Serikali kama mdau mkubwa wa huduma zinazotolewa kwa matumizi ya wananchi (Public Good) hususan tahadhari za hali mbaya ya hewa.

Kwa mabadiliko na maboresho hayo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajiwa kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini, hivyo sheria hii imehakikisha uwakilishi, ushirikishwaji, mabadiliko ya kimtazamo na uwajibikaji wa wadau wote ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na jumuiya za kijamii.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (katikati) akizinduwa rasmi Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), wengine ni wageni meza kuu katika hafla hiyo.

Mhandisi Isack Kamwelwe (Mb) ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, wizara inayoisimamia TMA, akitoa ujumbe wa Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa duniani mwaka huu, anabainisha kuwa ili kuhakikisha taasisi hiyo muhimu inatekeleza majukumu yake kiufanisi na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.

Serikali inaendelea kuijengea uwezo mamlaka ili iweze kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa lengo la kufuatilia mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mfupi na muda mrefu. Anasema taarifa za hali ya hewa ni muhimu sana katika kutoa maamuzi na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Anasema Serikali inatambua kuwa huduma za hali ya hewa husaidia na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na vilevile kuchangia katika maendeleo endelevu. Hivyo, kuliandaa taifa vizuri katika kukabiliana na maafa yanayosababishwa na vipindi vya ongezeko au upungufu wa maji kama vile mafuriko na ukame.

Waziri Kamwele anaongeza kuwa huduma za hali ya hewa zitolewazo husaidia watumiaji wa huduma hizo kupanga vyema shughuli zao ambazo ni pamoja na mipango ya utoaji wa huduma za maji mijini, kilimo, mifugo, maendeleo ya uvuvi, uzalishaji wa nishati na uratibu wa maafa miongoni mwa sekta nyingine.

“…Serikali inaendelea kuongeza uwezo wa TMA kufuatilia na kupima hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa matumizi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kufanya maamuzi ya mipango ya maendeleo katika sekta hizo.”
“Kwa kuzingatia hatua kubwa ya maendeleo iliyopigwa katika nyanja ya teknolojia na mahitaji yake katika sayansi ya hali ya hewa, Serikali inaipongeza TMA kwa kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma wanazotoa hapa nchini.” Anafafanua Mhandisi Isack Kamwelwe.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi (kushoto) akitoa utabiri wa  mwelekeo wa mvua za vuli, kwenye moja ya mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Huduma za Utabiri TMA, Dk. Hamza Kabelwa.

Aidha tangu kuingia kwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, TMA imeboresha zaidi utendaji wa kazi zake. Hii ni pamoja na utoaji wa huduma bora za hali ya hewa, hasa baada ya uwekezaji uliofanywa na Serikali kivifaa vya kisasa hususani katika kuboresha miundombinu.

Uwekezaji huu ni pamoja na ununuzi wa Rada za hali ya hewa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa nchini. Rada hizo zimefungwa Mwanza na Dar es Salaam na zingine tatu ziko katika hatua ya ununuzi ambazo zitafungwa  Mtwara, Mbeya na Kigoma.

Waziri aanasema Serikali itaendelea kuwekeza ili kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na maji kwa kuongeza uwezo wa wataalamu na miundombinu huku tukihimiza ushirikiano baina ya sekta mbalimbali zinazohusiana na zinazotumia huduma za hali ya hewa na rasilimali maji kwa lengo la kuendelea kuboresha maisha na ustawi wa jamii.
Hata hivyo anashauri jamii kuongeza kasi ya utumiaji wa huduma za hali ya hewa katika mipango yao na ile ya sekta zote za kiuchumi. Utekelezaji wa miradi ya kitaifa kama vile ujenzi wa miundombinu, uendelezaji na uzalishaji wa nishati inayotokana na maji, kilimo na rasilimali maji.

Nashauri pia tuendelee kuunga mkono juhudi za TMA katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwapa ushirikiano ikiwa pamoja na kuhakikisha wote wenye vituo vya hali ya hewa vinasajiliwa na TMA ili kwenda sambamba na matakwa ya sheria.
Akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani Machi, 23, 2020 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt. Agnes Kijazi anasema Ipo mifano halisi ya matukio ya hali mbaya ya hewa yaliyotokea nchini kwa mwaka 2019 na kuathiri upatikanaji na ubora wa maji katika baadhi ya maeneo.
Matukio hayo ni pamoja na kuchelewa kuanza kwa mvua za msimu wa Machi hadi Mei (masika), na matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika msimu huo ambapo mwezi Mei 2019 ulikuwa ni mwezi wenye mvua nyingi zaidi ya kawaida.

Moja ya rada zinazotumiwa na TMA kurahisisha kazi zake.
 Dkt. Kijazi ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, anaongeza kuwa matukio ya vimbunga Keneth na Idai katika msimu wa masika 2019, yamesababisha athari katika maeneo mbali mbali ya nchi ni miongoni mwa changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Kwa msimu wa mvua za mwezi Oktoba hadi Disemba (vuli) 2019 kumekuwa na mvua nyingi zaidi katika miezi ya Oktoba na Desemba.

“…Katika mwaka 2020 tumeshuhudia matukio ya mafuriko ya kutisha katika maeneo mbalimbali ya nchi hususan mkoani Lindi ambayo yalisababisha athari katika sekta mbali mbali ikiwa pamoja na sekta ya maji. Inatazamiwa kuwa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, matukio ya mafuriko na ukame yataongezeka kwa wingi (frequency) na ukubwa (intensity) na hivyo kusababisha athari katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya maji, nishati, usafirishaji na kilimo,” anaeleza nguli huyo wa masuala ya Hali ya Hewa ulimwenguni.

Pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na athari zake katika mfumo wa mzunguko na upatikanaji wa maji, taarifa za hali ya hewa za sehemu husika zitasaidia katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea upatikanaji wa maji.
Taarifa hizo ni pamoja na data za hali ya hewa za kipindi kirefu (klaimatolojia), utabiri wa hali ya hewa na matazamio ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate change projections).
Anabainisha kuwa TMA imeendelea kupata mafanikio katika kutekeleza mpango mkakati wake, ikiwa ni pamoja kuendelea kumiliki cheti cha ubora wa huduma kutoka Shirika la Viwango Duniani (ISO 9001:2015 Certification) katika huduma za hali ya hewa kwa sekta ya usafiri wa anga.

Kwenye mafanikio changamoto hazikosekani. Kwa sasa changamoto ni uhaba wa vituo vya uangazi wa hali ya hewa, mabadiliko ya matumizi ya teknolojia katika huduma za hali ya hewa, mahitaji ya taarifa za sekta maalumu na maeneo madogo madogo na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi katika misimu ya mvua ambayo husababisha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa.

Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2020, anatoa wito kwa wadau wa huduma za hali ya hewa kutoka sekta zote za kiuchumi na kijamii kuhakikisha wanazielewa na kuzitumia ipasavyo huduma za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi nchini.


No comments:

Post a Comment