Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Edward Mpogolo, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mpugizi Kata ya Mwaru wilayani humo juzi.
Na Dotto Mwaibale.
MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Edward Mpogolo amewaagiza maafisa Afya wa wilaya hiyo kupita kwenye maeneo yenye muingiliano wa kila siku wa watu, minadani na maegesho ya malori yaendayo nje ya nchi na yaingiayo nchini kukagua hatua za tahadhari za maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
Mpogolo alitoa maagizo hayo jana wakati akufungua Kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) na Viongozi wa Dini kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huo katika wilaya hiyo.
"Kwa kuwa wilaya yetu ya Ikungi imekuwa na mwingiliano mkubwa wa wageni hasa kupitia malori yaendayo nje ya Tanzania na mikoani nina waagiza maafisa Afya kupita kwenye maeneo yote ya biashara yenye mwingiliano wa kila siku wa wageni na kukagua hatua za tahadhari zinavyochukuliwa" alisema Mpogolo.
Mpogolo amewataka wananchi wote kufuatilia na kutii taarifa na maelekezo na makatazo yote kutoka mamlaka rasmi za Serikali na kuepuka taarifa za mitandaoni na simulizi kutoka kwa watu wasio na utaalamu kuhusu ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine Mpogolo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mpugizi Kata ya Mwaru amepiga marufuku kwa Waganga wa Tiba za Asili kuacha mara moja kuwapokea wateja wao kutoka maeneo mbalimbali ili kujiepusha na ugonjwa wa corona.
" Baadhi yetu tupo maeneo ya mpakani na wengine ni wataalamu wa tiba za asili mnawateja wenu kutoka nchi jirani za Kenya, Burundi, Rwanda na Ulaya chonde chonde nawaomba msiwapokee wageni licha ya kuwa na pesa nyingi" alisema Mpogolo.
Alisema kuendelea kuwapokea wageni hao huku taarifa zao zikiwa hazijulikani kunaweza kuhatarisha na kuenea kwa ugonjwa wa corona.
Mpogolo alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa kata hiyo mara watakapoona kuna mgeni kwenye maeneo yao wasisite kutoa taarifa na pia wakimuona mtu ana dalili za homa, kukohoa, kupiga chafya watoe taarifa haraka kwenye vituo vya Afya ili hatua za awali zichukuliwe .
Amewataka wananchi kuendelea kufuatilia kwenye vyombo vya habari taarifa ya serikali kuhusu ugonjwa huo wa COVID 19 badala ya kuangalia video kwenye mabanda na kucheza pool.
Mpogolo amewahakikishia wananchi kuwa wanaendelea kutekeleza maagizo ya Serikali ikiwa ni pamoja na kufunga shule zote za msingi na sekondari sambamba na kutoa matangazo na elimu mbalimbali ambapo pia amewaomba wazazi kuwahimiza watoto wao waliopo nyumbani kuacha kuzurura badala yake watumie muda huo wa likizo ya corona kwa ajili ya kujisomea.
No comments:
Post a Comment