SERIKALI imesisitiza kwamba nzige hawajaingia nchini Tanzania, tofauti na ilivyoripotiwa hapo awali
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro ambaye aliithibitishia BBC kuwa kundi la nzige limeonekana katika baadhi ya vijiji vya mjini Moshi, leo Jumatatu amesema kuwa nzige hao hawapo tena mkoani humo
''Asubuhi jana tuliambiwa kwamba wako kilometa 50 kutokea Mwanga kwa hiyo tukawasiliana na wenzetu wa Kenya upande wa Taveta wakatuambia kuwa hakuna, hao nzige kwamba hawajafika kwenye maeneo yao na kwa kuwa hawajafika kwao maana yake hawajafika kwetu kwa hiyo tukajiridhisha kwamba Mwanga hakuna, lakini ilipofika baadae jioni ikasemekana aina hiyo ya panzi au nzige wameonekana Moshi lakini walionekana kwa muda mfupi kisha baadae wakapotea''.
Katika kusisitiza hilo, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Italia George Kahema Madafa mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Flumicino Jijini Rome nchini Italia.
"Mimi nawahakikishia wakulima na wananchi wenzangu wa Tanzania kuwa kumekuwa na taarifa zinazoenea kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa nzige wa Jangwani nchini hususani mkoa wa Kilimanjaro siyo za kweli sisi tupo salama" alieleza Hasunga
Ameongeza kuwa hakuna taarifa za kitaalamu zilizothibitisha uwepo wa nzige kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Ila ni kweli Kuna nzige wameonekana Kaunti ya Kajiado nchini Kenya takribani kilomita 50 toka mpakani na Tanzania" Alisisitiza
Bwana Hasunga ameongeza kuwa Wataalam wa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo duniani (FAO) linaendelea na ufuatiliaji wa viashiria vya uwepo wa nzige na tayari hatua za awali za kuwadhibiti endapo wataingia nchini zimechukuliwa.
Aidha, amesema kuwa hatua hizo ni pamoja na Mashirika ya kimataifa ambayo Tanzania ni wanachama kuiahidi serikali ya Tanzania ndege tatu maalum za kunyunyizia dawa na uwepo wa dawa za tahadhali kwenye mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania Anna Mgwira amesema kundi hilo la Nzige lilionekena katika baadhi ya vijiji vya Moshi na kisha Wadudu hao wanaaminika kutokea upande wa nchi ya Kenya ambayo inapakana na Tanzania. Awali kulikuwa na taarifa zilizoenea katika mitandao ya kijamii na kusema kundi la nzige limeonekana umbali wa kilomita 50 kutokea mpaka wa Tanzania na Kenya.
Anna Mghwira anasema walipopata taarifa hizo asubuhi, waliangalia zaidi upande wa maeneo ya Taveta, lakini baadae taarifa zikaonyesha wameonekana katika baadhi ya vijiji vya Moshi."Sisi tulipopata hizo habari asubuhi, tukawa tunaangalia maeneo ya jirani yetu na Taveta, na ikaonekana upande ule hakuna, lakini jioni hii kumetokea taarifa zinazoonyesha kuwa maeneo ya Moshi hao nzige wameonekana kabisa sio kwamba wako km 50.
Wakati huohuo Maafisa wa Uganda wanasema kwamba nzige wameingia nchini humo kutoka Kenya, na kuthibitisha hofu zilizowasilishwa na maafisa wa UN kwamba wadudu hao waharibifu wataendelea kuenea katika eneo la Afrika mashariki.
Wadudu hao walidaiwa kupatikana katika eneo la mashariki la wilaya ya Amudat inayopakana na Kenya siku ya Jumapili.
Afisa wa kilimo katika wilaya ya Amudat awali siku ya Jumapili alidaiwa kusema kwamba wadudu hao walikuwa umbali wa kilomita 4 kutoka katika mpaka katika eneo linalojulikana kama Kiwawa nchini Kenya.
Kundi la nzige limeharibu eneo kubwa la mashamba na linatishia kuangamiza chakula katika eneo la Afrika mashariki.
Kenya tayari imeripoti mlipuko mbaya zaidi wa nzige katika kipindi cha miaka 70. Mabilioni ya wadudu hao tayari wameharibu makumi ya maelfu ya ekari za mimea nchini humo.
Mlipuko wa wadudu hao uliovunja rekodi pia uliripotiwa nchini Ethiopia na Somalia. Wadudu hao pia wameshambulia maeneo ya taifa la Sudan, Djibout na Eritrea.
Shirika la usalama wa chakula na kilimo katika Umoja wa mataifa FAO limetaja uvamizi huo wa nzige Afrika mashariki kuwa mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 25.
Nchini Somalia, serikali ilitangaza janga la dharura kutokana na uvamizi wa wadudu hao waharibifu.
Ilisema kwamba mlipuko huo ulikuwa unatoa tishio kwa hali mbaya ya ukosefu wa chakula. Ndege zimekuwa zikimwaga dawa za wadudu ili kudhibiti idadi ya nzige hao.
Lakini maafisa wamesema kwamba wana fedha chache na vifaa kukabiliana na wadudu hao katika maeneo yalioathirika.
Maafisa wa Umoja wa mataifa wanasema kwamba wana wasiwasi kwamba wadudu hao wanaweza kusambaa hadi Sudan kusini.
Wanakadiria kwamba takriban dola milioni 76 zinahitajika kwa sasa kuimarisha juhudi zinazolenga kuzuia kuenea kwa wadudu hao Afrika mashariki.
Nzige hao wa jangwani ambao wana urefu wa kidole cha mwanadamu huruka kwa makundi makubwa makubwa wakitafuta lishe.
Shirika la IGAD , limeripoti kwamba kundi moja la nzige huenda linashirikisha wadudu zaidi ya milioni 150 kwa mraba.
Limesema kwamba wadudu hao husafiri kupitia upepo na wanaweza kusafiri kwa zaidi ya kilomita 150 kwa siku.
-BBC
No comments:
Post a Comment