Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akisalimiana na baadhi ya viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Lusho mkoani Tanga.
|
Na Eleuteri Mangi, Tanga
SERIKALI inaendelea kuboresha usikivu wa matangazo ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa kuimarisha mitambo ya kurushia matangazo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kituo cha Mnyusi kilichopo Hale wilaya ya Korogwe na Kwemashai wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika wilaya za Korogwe, Lushoto pamoja na Halmashauri ya jiji la Tanga alipokuwa ziaraya kikazi kwa siku mbili mkoani humo kuanzia Januari 7-8, 2020.
Awali katika kikao na wadau wa habari jijini Tanga, Dkt. Mwakyembe alisema kuwa usikivu wa TBC Taifa mwaka 2015 ulikuwa ni asilimia 54 ambapo kwa sasa baada ya hatua mbalimbnali kuchukuliwa na serikali usikivu umefikia kiwango cha asilimia 73 na inatarajiwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020 utafikia zaidi ya asilimia 90 nchi nzima.
“Lengo la ziara yangu ni kukagua na kujionea utekelezaji na uboreshaji wa usikivu wa urushaji wa matangazo ya TBC ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao ya msingi ya Kikatiba ya kupata taarifa sahihi na kwa wakati” alisema Dkt. Mwakyembe.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara 18 (2) inabainisha kuwa “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”
Katika kutekeleza jukumu hilo Waziri Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Tanzania imefanya vizuri kwa kuhama kurusha matangazo ya Televisheni (TV) kutoka mfumo wa analojia na kuhamia mfumo wa kidijiti na kuifanya kuwa nchi ya kwanza Afrika hatua ambayo imesaidia wananachi kupata taarifa ya habari kupitia TV za ndani ya nchi bila gharama yeyote kupitia visimbuzi vyao.
Aidha, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa TBC ifanikiwa kupanua usikivu katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vitano katika wilaya za mpakani za Rombo, Tarime, Kibondo, Kakonko, Namanga, Nyasa hadi Mbambabay umekamilika. Wilaya za Ruangwa, Lushoto na Mtwara ambazo usikivu wake ulikua hafifu umeimarika na mkakati wa Serikali ni kujenga mitambo ya Redio katika mikoa ya Katavi, Njombe, Simiyu, Songwe, Unguja na Pemba.
Akimkaribisha Waziri Dkt. Mwakembe, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela alisema kuwa amefarijika kwa ziara hiyo mkoani humo kwani Waziri huyo amekuwa kiongozi wa kwanza kutembelea mkoa huo kwa mwaka 2020 na ziara ina manufaa kwa wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
“Mhe. Waziri, ziara yako kwetu ni muhimu sana itasaidia wananchi kuhabarishwa kwa kazi nzuri inayosimamiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na wewe unaendelea kuweka mazingira mazuri ya wananchi kupata habari kwa usahihi na kwa wakati” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Waziri Mwakyembe akiwa wilayani Lushoto, Mkuu wa wilaya hiyo Januari Lugangika amesema kuwa wilaya yake inabaadhi ya maeneo ambayo bado yana changamoto ya usikivu wa TBC yakiwemo Bumbuli, Mlalo pamoja na Umba, hali inayowanyima wananchi kupata haki yao ya msingi ya kupata habari kupitia chombo cha habari cha taifa.
Akitoa taarifa kwa viongozi hao kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la TBC, Mhandisi wa Ufundi Upendo Mbelle amesema kuwa shirika hilo linaendelea kuboresha usikivu wa TBC kwa kuweka mitambo midogo katika maeneo yenye usikivu hafifu ili kufikia maeneo ya mabondeni na sehemu zilizofichika nyuma ya milima.
Ziara ya kikazi ya Dkt. Mwakeyembe inahusisha mikoa ya kanda ya kaskazini katika katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na itahitimishwa mkoani Arusha.
No comments:
Post a Comment