WASAFIRISHAJI SASA KUFUATILIWA SAA ISHIRINI NA NNE - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 14 January 2020

WASAFIRISHAJI SASA KUFUATILIWA SAA ISHIRINI NA NNE

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eias Kwandikwa, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma, wakati Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ulipowasilisha Taarifa yake ya utekelezaji mbele ya Kamati hiyo.

SERIKALI
kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) imeanzisha utaratibu wa kufuatilia utendaji kazi wa mizani kwa saa ishirini na nne kwa kutumia mfumo wa kielektroniki na kamera za CCTV ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi wa mizani hizo na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu jijini, Dodoma.

"Mfumo huu umetuwezesha kugundua mwenendo mzima wa upimaji magari katika mizani kwani hata kama kuna vitendo vya rusha vimefanyika, basi mfumo unatusaidia kubaini vitendo hivi na inakuwa rahisi kuchukua hatua kwa yule aliyehusika”, amesema Naibu Waziri Kwandika.

Aidha, amefafanua kupitia mfumo huo suala la utunzanji wa barabara kupitia mpango wa udhibiti magari yaliyozidisha uzito nalo ni la uhakika kwani magari yaliyozidisha uzito yanaweza kubainika na kuchukuliwa hatua.

“Mathalani, katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba 2019, jumla ya magari 3,080,285 yalipimwa ambapo kati ya hayo, magari 19,432 yalikuwa yamezidisha uzito wa zaidi ya asilimia tano ya uzito unaoruhusiwa na kutozwa tozo ya uharibifu wa Barabara ambayo ni sawa na asilimia 0.63% ya magari yote yaliyopimwa”, amesema Naibu Waziri.

Ameongeza kuwa Wizara inaendelea kuelimisha wasafirishaji na wadau wengine kuhusu Sheria mpya ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016.

Kwandikwa ameeleza kuwa katika kuhakikisha Wakala unaendelea kusimamia kazi za udhibiti wa Uzito wa magari umeendelea kuweka mfumo wa kupima magari yakiwa kwenye mwendo ambapo kwa sasa mfumo huu tayari unafanya kazi katika vituo 13 na hivyo kupunguza msongamano wa magari katika mizani pamoja na muda wa kusafiri.

Naibu Waziri Kwandikwa ametaja kuwa baadhi ya vituo vya mizani vilivyofungwa mfumo  huu ni pamoja na Njuki (Singida), Nala (Dodoma), Wenda (Iringa) na Mpemba (Songwe).

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso, ameupongeza Wakala huo kuendelea kutekeleza miradi yake ambayo ina tija kwa Taifa na kusisitiza Wizara kuendelea kulipa madeni ya wakandarasi ili kuwezesha miradi mingine ambayo imesimama kuendelea kutekelezwa.

“Naomba Wizara muendelee kulipa madeni ya wakandarasi kwa kadri mnavyopata fedha kutoka Hazina, mkichelewa kulipa mnasababisha miradi kukwama na wananchi kukosa maendeleo”, amesema Mhe. Mwenyekiti

Katika hatua nyingine, Serikali kupitia Wizara hiyo imeamua kununua gari maalum litakalogharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ukaguzi wa barabara.
Gari hilo ambalo litakuwa la kisasa litaweza kukagua mtandao wote wa barabara kuu hapa nchini ndani ya mwezi mmoja na kutoa majibu ya ubora na mapungufu ya barabara kuanzia hatua za awali za ujenzi hadi mradi utakapokamilika.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, awali wakati akikagua mafunzo ya mfumo kwa watumishi wa Wizara, unaoonesha magari yanayopita kwenye mizani zote nchini na yale yanayozidisha uzito barabarani, amesema kuwa mfumo huo sio wa kuviziana au kutafuta mchawi au kuoneana wivu ila utasaidia kudhibiti wafanyakazi wa mizani na wasafirishaji wanaocheza na mizani hizo.
Amesema kuwa mfumo huo una lengo la kulinda miundombinu ya Taifa hususan barabara ili zisiendelee kuharibiwa pia utarahisisha kuona kila fedha inayotozwa kwa wasafirishaji.
“Mfumo huu ni wa kisasa na umeshaanza kutuletea majibu kwa kuwabaini wale watoa rushwa na wala rushwa katika mizani zetu hapa nchini”, amesisitiza Katibu Mkuu Mwakalinga.
Arch. Mwakalinga ametoa wito kwa wasafirishaji wote nchini kuhakikisha wanakuwa wazalendo na wanalinda miundombinu ya barabara kwa kutokuzidisha uzito wa mizigo na bidhaa wanayoibeba. 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment