Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akijibu swali bungeni Jijini Dodoma katika mkutano wa 18 wa Bunge la 11 ulioanza leo. |
Na Josephine
Majula na Saidina Msangi
SERIKALI imeahidi kuongeza jitihada za kuanzisha
matawi ya benki ya uhakika katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ili kuwawezesha wananchi kupata huduma
za kifedha kwa urahisi.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akijibu swali la Mbunge
wa Rufiji, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa aliyetaka kujua ni lini Serikali
itapeleka huduma za benki katika Wilaya hiyo.
Mhe. Mchengerwa alisema kuwa wananchi wa Jimbo kongwe
nchini wamekuwa wakipata tabu ya kupata huduma za kifedha hali inayowalazimu
kusafiri umbali wa Kilometa 100 kufuata huduma hizo.
Akijibu swali hilo, Dkt. Kijaji alisema kuwa wananchi
wa Rufiji waendelee kutumia huduma za fedha zilizopo wakati Serikali ikiendelea
kuboresha miundombinu muhimu pamoja na kufanya majadiliano na kuzishawishi
benki kuanzisha matawi yao katika Wilaya hiyo.
“Kufuatia mabadiliko ya Sekta ya Fedha nchini ya mwaka
1991, Serikali ilitoa uhuru kwa benki kufanya tafiti za kuamua kuhusu maeneo ya
kupeleka huduma za kibenki kulingana na taarifa za utafiti uliofanywa pamoja na
vigezo vya benki husika. Kwa kuwa benki zinajiendesha kibiashara maamuzi ya kufungua
tawi sehemu yoyote hapa nchini huzingatia vigezo hivyo”,alisisitiza Dkt. Kijaji.
Alisema Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa
huduma za kifedha hasa zile zinazotolewa maeneo ya karibu na wananchi, itaongea
na benki kuona namna ya kupunguza baadhi ya vikwazo vinavyoweza kusababisha
gharama za uendeshaji wa shughuli za benki wilayani hapo kuwa juu ili wananchi waweze
kupata huduma hizo kwa urahisi.
Alisema kwa sasa wananchi wa Wilaya hiyo wanapata
huduma za kifedha kupitia Kituo cha Makusanyo ya Fedha cha NMB (Cash
Collection Point - CCP) kilichopo katika Kata ya Utete pamoja na Mawakala
wa Benki, hususan Benki ya NMB na CRDB waliopo katika Wilaya ya Rufiji.
No comments:
Post a Comment