Pichani Daraja la Kerema maziwa katika barabara ya Kondoa-Bicha-Darai likiwa limekatika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Dodoma. |
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa (kulia) akikagua athari za uharibifu wa barabara na madaraja wilayani Kondoa, zilizosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Dodoma. |
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elias Kwandikwa (katikati) akikagua athari za uharibifu wa barabara na madaraja wilayani Kondoa, zilizosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Dodoma. |
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Mhe. Elius John Kwandikwa amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dodoma kufanya tathmini ya athari za mvua mkoani humo ili kuiwezesha Serikali kuanza ujenzi wa haraka katika barabara na madaraja yaliobomolewa kwa mvua zinazoendelea kunyesha.
Mhe. Kwandikwa amesema hayo baada ya kuona uharibifu wa barabara na madaraja wilayani Kondoa, ambapo amekagua barabara ya Kondoa-Bicha-Darai yenye urefu wa kilometa 25.6 na kujionea namna Daraja la Kerema maziwa linalounganisha Mji wa Kondoa na Kijiji cha Mrijo chini lilivyokatika.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri pia amekagua Barabara ya Kondoa-Katesh ambayo mawasiliano yamekatika kufuatia kusombwa kwa Daraja la Mngulwi, ambapo amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua ili kuepusha maafa.
"Uongozi wa Wilaya shirikianeni na Tanroads kupata ufumbuzi wa muda ambao ni salama wakati Serikali ikijipanga kuchukua hatua za kudumu kuimarisha miundombinu hii," amesema Mhe. Kwandikwa.
Aidha Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dodoma Eng. Leonard Chimagu amewataka wananchi kutumia njia mbadala ili kuepuka maafa na kuacha shughuli za kilimo pembeni mwa mito ili kulinda kingo za mito wakati mvua zikiendelea.
No comments:
Post a Comment