Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA), Prosper Magali (kulia) akizungumza kwenye warsha ya wanachama na wadau wa Jumuiya hiyo iliyofanyika sambamba na maonesho. |
JUMUIYA ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) imeiomba serikali na wadau wote wa usambazaji umeme kutengeneza mpango mkuu wa usambazaji umeme utakaoshirikisha sekta ya miradi midogo ya uzalishaji na usambazaji umeme utakaotenga na kuweka wazi maeneo ambayo wawekezaji binafsi watafanya shughuli zao bila kuwa na wasiwasi na mwingiliano na shughuli za usambazaji umeme zinaziofanywa na serikali kupitia REA.”
Ushauri huo umetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA), Prosper Magali wakati wakimwelelezea Waziri wa Biashara na Viwanda, Innocent Bashungwa kupitia risala ya TAREA katika hafla ya kufunga Maonesho ya siku mbili ya Nishati Jadidifu Tanzania yaliyofanyika Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“TUKIWA wadau wa kuisaidia serikali kuwafikishia wananchi huduma za nishati hasa wa vijijini, mara zote kabla hatujaamua kuchagua eneo la kupeleka huduma, tunapenda kupitia na kuelewa mipango ya usambazaji umemem, ili twende maeneo ambayo ni gharama kubwa au ni vigumu kwa serikali kufikisha umeme.”
Alisema inatokea wakati mwingine, mipango hubadilika na kujikuta miundombinu ya REA inafikishwa maeneo ambayo tayari yana miradi binafsi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme...ilahi bado kuna maeneo mengi yanayohitaji huduma hizo na hayajafikiwa.
‘‘Tunaiomba serikali na wadau wote wa usambazaji umeme kutengeneza mpango mkuu wa usambazaji umeme utakaoshirikisha sekta ya miradi midogo ya uzalishaji na usambazaji umeme utakaotenga na kuweka wazi maeneo ambayo wawekezaji binafsi watafanya shughuli zao bila kuwa na wasiwasi wa mwingiliano na shughuli za usambazaji umeme zinaziofanywa na serikali kuptia REA.”
Makamu Mwenyekiti huyo wa TAREA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho hayo mwaka huu, alisema sababu kubwa ya kuwapo kwa bei kubwa za tozo za umeme kwenye miradi ya nishati jadidifu ni gharama kubwa za uwekezaji zisizowiana na mapato madogo yatokayo kwenye mauzo ya umeme kwenye miradi hiyo.
Aliitaja changamoto nyingine zinazowakabili waendelezaji binafsi wa miradi ya nishati jadidifu hasa wa ndani kuwa ni ugumu wa kupata mitaji ya kuendeleza na kufanyia shughuli zao kwa muda mrefu.
“Changamoto kubwa imekuwa taratibu na masharti magumu yaliyowekwa na mabenki haya yanayokwamisha waendelezaji binafsi kufikia fedha za kuendeleza miradi. Tunaamini serikali inaweza kusaidia kuitazama changamoto hii na kutafuta njia na majawabu yatakayowezesha kuwa na taratibu wezeshi kwa waendelezaji wadogo kufikia fedha hizi,” alisema.
Katika banda la TAREA, Katibu wa Rasalimali Watu, Cecilia Richard alimwambia Waziri Bashungwa kuwa kazi kubwa ya TAREA yenye zaidi ya wanachama 700 ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu nishati jadidifu kupitia makongamano, vyombo vya habari na mafunzo kwa vitendo kwa wadau mbalimbali.
Kwa upande wake, Waziri Bashungwa aliyemwakilisha Waziri wa Nishati, Merdadi Kalemani alizihimiza kampuni zinazojihusisha na uzalishaji mdogonna usam,bazaji wa umeme kwa kutumia teknolojia ya nishati jadidifu kuwahimiza wenye viwanda vya bidhaa wanazotumia kuja Tanzania kuwekeza viwanda vyao nchini kwani tayari kuna soko kubwa na la uhakika.
Alisema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya Watanzania kuhusu nishati jadidifu, soko la bidhaa za nishati hiyo limekuwa hivyo, ni vema wawekezaji kujenga viwanda Taania ambapo tayari kuna soko linalokua kwa kasi na la uhakika.
“Hapa Tanzania teknolojia ya nishati jadidifu inazidi kusambaa na kila siku soko la vifaa hivi linaongezeka, lakini vifaa vingi vinaagizwa kutoka nje ya nchi, Hivyo basi wambieni wazalishaji Tanzania njooni tuweke viwanda karibu na soko. Tanzania kuna soko kubwa, la uhakika na linolokua kwa kasi,” alisema Waziri.
Alisema uwekezaji huo utakuza soko hata katika nchi za jirani. “Nishati ya kuaminika na endelevu ni kitu kisichoepukika kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa lolote duniani hasa tunapoelekea kufikia lengo la Uchumi wa Viwanda ifikapo mwaka 2025.”
“Pamoja na Lengo hili, mafanikio katika sekta zote za uchumi, huduma za jamii na maendeleo yanategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa kuaminika na endelevu wa nishati ya kutosha.”
Waziri Bashungwa alisema changamoto iliyopo wadau kushirikiana kushughulikia masuala yote yanayokwamisha upatikanaji rahisi, ueneaji na ongezeko la matumizi ya nishati hizi kwa wananchi wote hasa walioko vijijini.
“Kuweni tayari kupeleka huduma zenu vijijini kwa kuanzisha matawi ya biashara zenu badala ya kunga’ng’ania mijini. Hii itapunguza gharama kubwa ya kufuatilia teknolojia hizi na ufundi unaohitajika ili zitumike kwa ubora unaokubalika kitaalam,” alisema Waziri.
Pamoja na hayo, Waziri huyo ameziagiza mamlaka na taasisi zote wadau zilizo chini ya Wizara ya Nishati, Ofisi ya makamu wa rais (Muungano na Mazngira) na Wizara ya Bishara na Viwanda zikiwamo Taasisi ya Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda nchini (TIRDO), Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO),TAREA, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), na CARMATEC, na Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Nishati na Maji (EWURA) kukutana kuweka mpango utakaobainisha changamoto zinazoikumba teknolojia ya nishati jadidifu na ufumbuzi wake.
Magali ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa TAREA na Kaimu Mkurugenzi wa REA, Amosi Maganga walisema wameyapokea maelekezo ya Waziri na watayafanyika kazi haraka kwa kuwa dunia nzima inajikita katika matumizi ya nishati mbadala.
No comments:
Post a Comment