Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akipanda mti kama shughuli maalumu ya sehemu ya kumbukizi ya maadhimisho ya sherehe za uhuru kwa mwaka 2019 mkoani Singida jana.
Wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa chama na Serikali wakiwa wameshikilia miche ya miti mbalimbali ikiwemo ya matunda kabla ya zoezi la kuanza kuipanda kwenye viunga vya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za uhuru kwa mwaka 2019 mkoani Singida.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akizungumza kwenye maadhimisho ya sherehe za uhuru kwa mwaka 2019 mkoani Singida.
Askari wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida wakishiriki kwenye shughuli ya kupanda miti kama shughuli maalum ya sehemu ya kumbukizi ya maadhimisho ya sherehe za uhuru kwa mwaka 2019 mkoani humo.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick, akipanda mti.
Zoezi la upandaji miti likiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (kushoto) akimkabidhi Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick pesa taslimu kiasi cha shilingi 180,000 kwa ajili ya kuwapatia watoto wote waliozaliwa kwenye kumbukumbu ya siku ya uhuru kwa mwaka huu ndani ya Manispaa ya Singida.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victorian Ludovick akikabidhi zawadi kwa mmoja wa wazazi waliojifungua siku ya maadhimisho ya uhuru, jumla ya watoto 12 waliozaliwa siku hiyo ndani ya Manispaa ya Singida walipatiwa zawadi mbalimbali.
Na Mwandishi Wetu, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi ameongoza mamia ya wananchi wa mkoa huo katika zoezi la kupanda miche mbalimbali ya miti zaidi ya 300 ikiwemo ya matunda, ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya maadhimisho ya siku ya uhuru kitaifa mkoani humo, kwa mwaka huu.
Shughuli hiyo ilianza mnamo majira ya saa 2 asubuhi kwa wananchi na viongozi wa dini, vyama vya siasa na serikali kukusanyika katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ‘Mandewa’ kabla ya kuanza kwa zoezi hilo la upandaji miti lililodumu kwa takribani masaa 3.
Akizungumza kwenye eneo hilo, Dk Nchimbi alisema taifa lolote la watu wabunifu, wazalendo na wawajibikaji ni lazima kwanza kuzingatia uwepo mazingira safi na salama yanayozunguka pande zote.
Alisema haikubaliki hata kidogo kwa baadhi ya watanzania kuendelea kukata miti kwa kisingizio cha kutafuta fedha au kujiajiri, huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kukosa uzalendo.
“Kwa maadhimisho haya sote tukubaliane kuanzia sasa kukata miti iwe basi…kiasi cha mkaa kinachokatwa Singida ni kikubwa, inasikitisha sana kuendelea kuona uharibifu huu mkubwa wa mazingira ukiendelea kufanywa ndani ya mkoa wetu,” alisema Nchimbi.
Aliwataka wanasingida kuendelea kushikilia kauli mbiu iliyozoeleka ya mkoa huo ya ‘Achia Shoka kamata Mzinga’ kama sehemu ya kutunza misitu kwa ustawi wa afya ya mazingira na kiini cha ufugaji na uzalishaji wa mazao ya nyuki kwa maendeleo ya uchumi wa kaya na Taifa.
Akizungumzia kuhusu zao la korosho, Dk. Nchimbi alisema zao hilo ni fursa ya kipekee ndani ya mkoa wa Singida kwa sasa, kwani ndani ya mda mfupi ujao linakwenda kubadilisha kabisa uchumi wa mkoa huo kutokana na wataalamu kuthibitisha kuwa zao hilo lenye thamani kubwa kuwa ni rafiki kwa ardhi ya mkoa huo.
“Tusichelewe kuifikia fursa hii itakayotusaidia kuimarisha uchumi wetu, hivyo naagiza kuanzia sasa kila mtendaji afanye sense ya vijana waliopo kwenye maeneo yao, na hatimaye nataka kila kijana awe na walau nusu heka ya shamba la mkorosho,” alisema Nchimbi.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Deogratias Banuba, alisema idadi ya miti hususani ya matunda iliyopandwa kupitia maadhimisho hayo italeta manufaa makubwa kwa ulaji na ustawi wa afya ya wagonjwa watakaoendelea kuletwa kwa matibabu hospitalini hapo.
Dk. Banuba ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Upasuaji, akizungumzia kuhusu miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli ndani ya sekta ya afya, alisema kwa sasa huduma zimeboreshwa sana ikilinganishwa na hapo awali.
Alisema kwa upande wa huduma za upasuaji hasa kwenye eneo lake la mifupa huduma zote tena kwa kiwango cha juu kwa sasa zinafanyika ndani ya mkoa huo, huduma zimeboreshwa, vifaa tiba vyote muhimu kwa ajili ya mifupa vinapatikana tena kwa wakati.
Banuba alisema zamani walikuwa wakilazimika kuwapa rufaa wagonjwa ya kwenda kutibiwa hospitali za Dodoma au Muhimbili, lakini tokea mheshimiwa Rais Magufuli aliposhauri Hospitali zote za Rufaa za mikoa zihamie Wizara ya Afya hakika kumekuwa na mabadiliko makubwa sana, hasa eneo la kibingwa.
“Sasa tuna huduma za upasuaji upande wa akinamama na kila eneo, kiukweli singida kwa sasa tupo vizuri kwenyeupande wa sekta ya afya, na bado tunaendelea kuimarika zaidi kwa utoaji wa huduma bora na za viwango vya juu,” alisema Dk Banuba.
Awali Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida (DAS), Wilson Shimo, alisema ukiachilia mbali zoezi la upandaji miti lililooongozwa na Mkuu wa Mkuu wa Mkoa huo, kupitia tukio la kumbukizi hiyo ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika, na 57 ya Jamhuri ya Muungano aliwataka wakazi wa mkoa huo kuwa makini na kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua.
“Niwasihi wananchi wote mnaoishi mabondeni, maeneo ambayo ni oevu, chepechepe wachukue tahadhari ya kuondoka kwenye maeneo hayo, sambamba na kuwa karibu na watoto wadogo kwa kuepuka kuwaachia kutembea kwenye maji yanayotiririka au mito inayotembea kwa kasi au mashimo yaliyochimbwa kwa kina kirefu, ambayo yanaweza kuleta athari ya watoto kutumbukia na kusababisha vifo,” alisema.
Alisema kwa neema ya mvua zinazoendelea kunyesha, aliwasihi wakulima kuendelea kutumia mvua zilizopo kulima kilimo cha kitaalamu kwa kuzingatia tija.
No comments:
Post a Comment