Na Eleuteri Mangi, Dodoma
WAAJIRI wametakiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha watumishi wanashiriki katika michezo na kufanya mazoezi maeneo yao ya kazi.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza leo wakati wa ufunguzi wa tamasha la michezo la wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyo ambukiza linalofanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo kilele chake ni Novemba 14, 2019 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jahuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Mjaliwa.
“Mnaweza kuanzisha timu mbalimbali za michezo na kutenga siku maalum katika mwezi kwa ajili ya mabonanza ya michezo kwa kuweka mazingira rafiki ya kufanyia mazoezi kazini kwa kununua vifaa na kutenga vyumba vya mazoezi. Hii itaimarisha afya za watumishi na kupunguza gharama za matibabu katika taasisi husika.” Naibu Waziri Juliana Shonza.
Naibu Waziri Shonza amesema kuwa tamasha hilo linalenga kuhamasisha wananchi kushiriki katika michezo mbalimbali na mazoezi ya viungo ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka hapa nchini.
Magonjwa yasioyoambukiza hutokana na mitindo isiyofaa ya maisha kama matumizi ya tumbaku, lishe duni, matumizi ya pombe kupita kiasi, pamoja na kutoshughulisha mwili au kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara.
Magonjwa hayo ni kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na mishipa, saratani, pumu na magonjwa ya akili ambayo yamekuwa sugu na yana gharama kubwa za matibabu ambapo amesema kuwa watu wengi hufikiria mazoezi ni lazima ukimbie au ucheze mpira, la hasha. Mazoezi ni jambo lolote linalohusisha misuli na kusababisha kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kasi ya kupumua.
Wataalam wa afya wanasema kuwa kiwango cha mazoezi kinacholeta faida ni mazoezi yasiyopungua dakika 30 kwa siku angalau siku tatu kwa wiki na yanayomfanya mtu kutokwa na jasho.
Aidha, Naibu Waziri amesisitiza kuwa kupitia tamasha hilo, ufanyike uhamasishaji wa watu kupima afya hususani wa magonjwa yasiyoambukiza. Tiba ya mapema inapunguza uwezekano wa kupatwa na madhara zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chemba Saimon Odunga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amewakaribisha washiriki wa tamasha hilo mkoani Dodoma ambalo limeshirikisha washiriki kutoka ndani na nje ya mkoa huo na hata nje ya nchi.
Odunga amewataka wakazi na wananchi wa mkoa wa Dodoma kutumia fursa ya tamasha hilo kwa kushiriki michezo mbalimbali hatua ambayo itwasaidia watu na jamii nzima kuweka afya zao katika hali bora ambayo inawatenga na magonjwa yasiyoambukiza.
Tamasha hilo ni la wiki moja ambalo limeandaliwa na kuratibiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma, pamoja na Wizara ya Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo limeshirikisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, pete, kikapu pamoja mchezo wa kuvuta kamba. Tamasha hilo linaongozwa na kauli mbiu yetu ya mwaka huu; “Tutembee Pamoja Katika Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza”
No comments:
Post a Comment