Mkuu wa Programu TGNP Mtandao, Shakila Mayumanga akiwasilisha mada katika maadhimisho hayo. |
Sehemu ya washiriki katika Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yalioandaliwa na TGNP Mtandao na kushirikisha asasi, vikundi anuai wadau wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia. |
MC wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yalioandaliwa na TGNP Mtandao na kushirikisha asasi, vikundi anuai wadau wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia akiratibu mazungumzo. |
Na Mwandishi Wetu
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imewataka wadau mbalimbali wa kupinga ukatili wa aina yote kuuunga mkono Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWA) ili uweze kufanikiwa.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Nyanda Shuli alipokuwa akizinduwa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yalioandaliwa na TGNP Mtandao na kushirikisha asasi, vikundi anuai wadau wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Alisema mpango huo ni muhimu kwani umelenga kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022, hivyo kuwataka wadau wa kupambana na ukatili wa kijinsia kuutumia na kuuunga mkono ili kutokomeza vitendo vya ukatili kwa kundi hilo.
Mpango huu ambao umekwisha anza utekelezaji wake unalenga kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022, nitoe rai kwa wadau mbalimbali wanao pambana na ukatili dhidi ya kundi la watoto kutumia mpango huu katika shughuli zao kama sehemu ya kuweka nguvu za pamoja kwenye mapambano ya ukatili wa kijinsia," alisema Kamishna Shuli akizungumza.
Aidha alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, itaendelea kushughulikia kikamilifu matukio yote ya uvunjifu wa haki za binadamu pale yanapowafikia na kuwaomba wadau anuai kushirikiana ili kuhakikisha wanafanikiwa kwa pamoja.
Awali akizungumza katika hotuba yake kwenye maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Bi. Lilian Liundi alisema licha ya juhudi ambalimbali zinazofanywa na Serikali ukatili wa kijinsia bado ni janga la kitaifa.
"...Na hali hii si kwa Tanzania pekee bali mataifa ya Kiafrika. Tunashuhudia vifo vingi, ulemavu, udhalilishaji, udunishaji wa utu wa wanawake, wasichana na watoto kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ukiwemo ubakaji," alisisitiza Bi. Liundi.
Alisema kama seluthi moja ya wanawake wanakumbana na ukatili kutoka kwa wenzi au marafiki na kama tungeliweza kufanya utafiti na kuhesabu jinsi taifa linavyopata hasara ya kiuchumi tungetangaza rasmi kuwa ukatili ni janga la kitaifa, hivyo viongozi wa juu hadi wa chini wangelikemea na kuweka mikakati madhubuti zaidi ya kuhakikisha ukatili unakuwa historia.
Hata hivyo alisema kila mmoja akiwa na nia na kutekeleza majukumu yake ipasavyo vitendo vya ukatili vinaweza kutokomezwa na kushauri mipango ya kibunifu na kisasa inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na vitendo hivyo.
Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP Mtandao yaliambatana na mijadala mbalimbali kwa wadau pamoja na uwasilishaji mada kwa wanajopo kuangalia namna ya kukabiliana na hali ya vitendo vya unyanyasaji.
No comments:
Post a Comment