SUMUKUVU AINA YA “AFLATOXIN” YASABABISHA VIFO 8 NCHINI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 8 November 2019

SUMUKUVU AINA YA “AFLATOXIN” YASABABISHA VIFO 8 NCHINI

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhandisi Tumaini Magesa akifungua semina ya kuelimisha wadau wa kilimo na mifugo wa Mkoa wa Manyara kuhusu udhibiti wa tatizo la sumukuvu.Semina imefanyika Kiteto  kupitia mradi wa TANIPAC.

WATU
nane wameripotiwa kufariki dunia kutokana na kula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu kwenye mikoa ya Manyara na Dodoma mwaka huu.
Kauli hii imetolewa Novemba 8, 2019 na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhandisi Tumaini Magesa wakati akifungua semina ya kuelimisha wadau juu ya mikakati ya serikali katika kudhibiti tatizo la sumukuvu
Amesema mkoa wa Manyara  umekuwa na tatizo la sumukuvu takribani miaka mitatu sasa ambapo vifo vimeendelea kutokea kwa watu kutokana na  kula chakula kilichoathirika na kuvu.
“Jumatatu iliyopita (04.11.2019) katika kijiji cha Kimani hapa Kiteto mtoto mdogo amefariki dunia na wengine wamelazwa hospitalini Dodoma kutokana kula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu” alisema Mkuu wa Wilaya 
Mhandisi Magesa aliendelea kusema katika mwaka huu 2019 zaidi ya watoto sita (6) wamefariki dunia katika wilaya ya Kiteto pekee takwimu hizi hazijajumuisha watu wazima,hali hii inatarisha usalama wa maisha ya watu 
Mkuu huyo wa wilaya ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuandaa semina hii kwa mkoa wa Manyara na kuongeza kuwa “wananchi wetu wakifahamu namna ya kujiepusha na tatizo la sumukuvu itasaidia kuwa na Taifa salama” hususani vijijini. 
Ili kukabiliana na tatizo la sumu kuvu nchini,Wizara ya Kilimo kupitia Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) imeanza kutoa mafunzo kwa wadau katika mikoa iliyoathiriwa zaidi na sumukuvu ili kuwajengea uwezo wa kudhibiti tatizo hili.
Mratibu wa mradi wa TANIPAC Clepin Josephat  alieleza maana ya Sumukuvu kuwa ni aina ya sumu inayozalishwa na kuvu (fangasi) wanaoshambulia zaidi mazao ya mahindi na karanga.
Clepin aliongeza kuwa kuvu wanaosababisha sumukuvu huonekana kwa rangi ya kijani,chungwa ,kijivu na au njano.
Aliongeza kusema  utafiti ulifanyika mwaka 2016 ulionyesha kuwa ,tatizo hili linachangiwa zaidi na wakulima nchini kutozingatia kanuni bora za Kilimo mfano kuvuna mahindi ambayo hayajakauka vizuri na kwenda kuyahifadhi ghalani hupelekea fangasi wa kuvu kuyaathiri.
Akitoa mada katika semina hiyo Frolence Evaristi  mtaalam toka Kitengo cha Dharura na Maafa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto alisema madhara ya muda mrefu  kwa mtu anapokula chakula kilichochafuliwa na sumukuvu (Alfatoxin) hupekea saratani ya ini,figo na koo pia huathiri ukuaji wa watoto chini ya miaka mitano (udumavu)
Aliongeza kusema mwaka huu Juni kulitokea vifo Nane (8) kati ya watu 60 waliogundulika kuathirika na sumukuvu kwenye mikoa ya Dodoma na Manyara .
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Japhet Nkangaga alisema sumukuvu inathiri mifugo kutokana na kula chakula kilichochafuliwa na kuvu.
Ametaja madhara kwa wanyama kama ng’ombe,mbuzi au kuku kudumaa na kuzaa ndama waliothirika na kuvu hali inayopelekea mifugo kufa na hasara kwa mfugaji.
Wizara ya Kilimo inatekeleza mradi wa kudhibiti sumukuvu kwenye mikoa 10 Tanzania Bara na pia Zanzibar kwa gharama ya shilingi Bilioni 45 kwa kuhamasisha matumizi sahihi ya kanuni bora za Kilimo ili kuboresha afya ya mimea. 

Serikali imedhamiria kuhakikisha elimu ya kukabiliana na sumukuvu ili kuzuia vifo inawafikia wananchi kwenye mikoa iliyoathiriwa zaidi Tanzania Bara na Visiwani.

No comments:

Post a Comment