NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu jana amefanya ziara ya kutembelea sehemu ya Shamba la miti Sao Hill lilipo wilayani Mufindi mkoani Iringa ambalo limeathiriwa na moto. Moto huo uliotokea mwishoni mwa wiki katika kipindi cha siku sita na umeathiri zaidi ya hekta 1000 za miti likiwemo shamba hilo la Serikali pamoja na mashamba mengine ya Taasisi zingine na watu binafsi.
Katika shamba hilo pekee jumla ya hekta 600 za miti aina ya misindano na mikaratusi imeathirika na moto huku vyanzo vya moto huo vikidaiwa kuwa ni wananchi kuandaa mashamba kwa ajili ya kilimo, urinaji wa asali pamoja na shughuli za uvunaji miti.
Mbali ya hasara hiyo, Moto huo pia umeleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kumuunguza mtumishi wa kiwanda cha Sao Hill alipokuwa katika jitihada za kuzima moto huo. Moto huo umeteketeza gari aina Isuzu Lori. mizinga ya nyuki 24 kati ya 83, mbao, magogo pamoja na mashine za kuchania mbao zilizokuwemo katika shamba hilo.
Akizungumzia kuhusu hasara hiyo, Naibu Waziri Kanyasu amesema moto huo umesababisha hasara ya zaidi ya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni tano huku ukiwaacha wananchi waliokuwa na mashamba ya miti kwenye wakati mgumu. Amesema kwa mwaka jana pekee Shamba hilo la miti la Sao Hill, moto huo uliunguza hekta 400 za miti na hivyo kusababisha hasara ya zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 1.
Kufuatia hali hiyo Waziri Kanyasu ameuagiza Uongozi wa Shamba hilo kuiuza haraka miti iliyokuwa imefikia umri wa kuanzia miaka 10 hadi miaka 27. Amesema taratibu hizo zifanyike haraka kwa vile miti iliyoungua kwa moto ikiendelea kubaki kama ilivyo huharibika kwa haraka na hivyo kupelekea kutokufaa kwa mbao.
Hata hivyo, Mhe. Kanyasu amesema licha ya kuwa miti hiyo itauzwa, Shamba hilo limepata hasara kubwa kwa vile sehemu kubwa ya miti iliyoathiriwa na moto ni yenye umri wa miaka mitatu ambayo haiwezi kutumika kwa matumizi yoyote.
Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri Kanyasu ameutaka Uongozi wa wilaya ya Mufindi kuandaa sera itakayowazuia wananchi kuandaa mashamba yao katika kipindi cha msimu wa kilimo kwa kutumia moto ili kuzuia hasara kubwa inayotokea kila mwaka.
Aidha, Ameuagiza Uongozi wa shamba hilo kuja na mkakati mpya wa namna ya kukabiliana na janga hilo la moto ikiwa ni pamoja na kuandaa kingo zenye ukubwa wa kutosha kati ya shamba moja na jingine ili kuzuia moto endapo utaweza kutokea usiweze kuathiri sehemu kubwa ya miti.
''Matukio haya ya moto yanayotokea kila mwaka inabidi yatufundishe namna ya kuweza kukabiliana nayo, tusipotaka kujifunza mwakani tutapoteza hekta nyingi zaidi,'' alisisitiza Kanyasu.
Amesema licha ya kuwa inaonekana kulikuwa na maandalizi ya kutosha kutoka kwenye vikosi vya kuzuia moto lakini hata hivyo kuna haja ya kutumia teknolojia mpya ya namna ya kupambana na moto huo uliounguza hekta 1000 kwa muda wa masaa mawili.
Akizungumzia kuhusu hatua zilizochukuliwa hadi hivi sasa za kukabiliana na majanga ya moto katika shamba hilo, Mhe. Kanyasu amesema licha ya kuwa shamba hilo limeagiza gari la zima moto lenye thamani ya kiasi cha shilingi milioni 800 lakini hata hivyo kutokana na jiografia la eneo hilo halitaweza kuleta ufanisi.
kwa upande wake Kaimu Meneja wa Shamba hilo, Sillima Kombe amesema ili kukabiliana na majanga hayo ya moto katika shamba hilo la Sao Hill lenye ukubwa hekta 135,903 linahitaji ndege zisizo na rubani tatu, Helikopta 3 pamoja Darubini za kisasa 20.
No comments:
Post a Comment