Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua maadalizi ya Ofisi za muda za Halmashauri ya Mtama mkoani, Lindi, Oktoba 17, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
|
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ofisi za muda za Halmashauri ya Mtama na kusema ameridhika na maandalizi aliyoyakuta. Ametoa kauli hiyo Oktoba 17, 2019 wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri hiyo pamoja na wazee wa kijiji cha Mtama kwenye ukumbi wa mikutano jirani na ofisi ya mbunge wa jimbo la Mtama.
"Nimeridhika na jitihada zenu za kuja kuandaa ofisi na kufanya usafi ili kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais. Lakini pia nimefarijika na uamuzi wenu wa kujitolea eneo la ekari 100 la kujenga Halmashauri yenu," amesema.
Amewataka watumishi hao wahamasishe ujenzi wa nyumba bora na kuhimiza usafi kwenye makazi ya watu ili mji wao uendane na hadhi ya makao makuu ya wilaya.
Hamasisheni ujenzi wa nyumba bora ili pawe na nyumba zenye muonekano wa Halmashauri mpya. Lakini Bwana Afya simamia usafi kuanzia stendi kule.
Halmashauri sasa pimeni viwanja. Pato la ndani la Halmashauri yenu mtalipata kwa kupima viwanja sababu vinauzika. Lazimapawe na mpangilio wa makazi, majengo kadhaa na maeneo ya biashara," amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amemwagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Lindi, Bw. Thomas Safari asimamie vizuri fedha za wilaya hiyo ili baadhi ya watumishi wasifuje fedha za Halmashauri.
"Hakikisha watu hawatumii fursa hii kufuja fedha za Halmashauri. Hamisha fenicha watu waanze kazi hapa. Tunahamisha Halmashauri kuja hapa, watumishi msilale Lindi, bali mlale Mtama."
Naye Mbunge wa Mtama, Bw. Nape Nnauye alimweleza Waziri Mkuu kwamba tangu Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli atoe agizo la kuhamishia makao makuu ya Halmashauri ya Mtama hapo Mtama, wamekuwa na vikao mbalimbali na wamefanikiwa kupata ekari 100 ambazo wananchi wamejitolea bure.
"Tumekuwa na vikao mbalimbali na jioni tutakuwa na kikao na wazee wa hapa ili kuwajulisha mchakato mzima. Kesho tutakuwa na mkutano mkubwa na wananchi. Lengo letu ni kuhakikisha tunapunguza gharama kwa kiasi kikubwa," alisema.
No comments:
Post a Comment