Na Mathias Canal, Songwe
MASHINDANO ya "HASUNGA
CUP 2019" tarehe 29 Septemba 2019 yamefika ukomo Wilayani Mbozi
Mkoani Songwe ambapo timu ya Hasamba Fc ndiyo iliyoibuka kidedea na
kunyakua zawadi kwa kuibamiza bila huruma timu ya Ihanda Fc kwa jumla ya Penati
7 kwa 6.
Timu hiyo ya Hasamba Fc imeambulia ushindi huo wa
goli 7 kwa 6 mara baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika kwa timu hizo kutoka
suluhu magoli yaliyofungwa na mshambuliaji Asili Mnkondya wa timu ya Ihanda
mnamo dakika ya 20 huku Beny Mgonde akiisawazishia timu yake mnamo dakika ya 72
ya mchezo huo.
Michuano hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa
Vwawa na kuendeshwa kwa umahiri mkubwa, ilizinduliwa mwezi Machi 2019 katika
uwanja wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Songwe huku ikizikutanisha timu 18
zilizotokana na muunganiko wa timu za vijiji katika kata hizo 18 katika Jimbo
la vwawa.
Akizungumza katika kilele cha Mashindano hayo
kilichofikia ukomo katika katika viwanja wa Chama Cha Mapinduzi Mkoani Songwe, Mbunge
wa Jimbo la Vwawa ambaye pia ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema
kuwa mashindano hayo yalianzishwa kwa lengo mahususi kwa ajili ya kubaini
vipaji vya vijana kwa ajili ya kuunda timu itakayoshiriki ligi daraja la nne na
hatimaye ligi kuu Tanzania bara.
Amesema kuwa mashindano hayo pia yamekuwa ni sehemu
ya kuhamasisha wananchi pamoja na wadau mbalimbali ambayo yamewaimarisha vijana
hususani katika kuonyesha vipaji vyao.
Katika mashindano hayo Mshindi wa kwanza ambayo ni
timu ya Hasamba Fc amekabidhiwa zawadi ya Seti moja ya jezi, Seti moja ya soksi
na kitita cha Shilingi laki tatu.
Mshindi wa pili timu ya Ihanda Fc imepewa zawadi seti moja ya jezi, seti moja ya soksi na kitita cha shilingi 200,000, Mshindi wa tatu yeye amekabidhiwa seti moja ya jezi na kitita cha Shilingi 100,000 huku mshindi wan ne akijinyakulia seti moja ya jezi pekee.
Katika hotuba yake Mbunge huyo wa Jimbo la Vwawa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga aliwapongeza viongozi wote na timu zote zilizoshiriki ligi hiyo kwani bila wao kusingekuwa na mafanikio yenye tija.
Mhe Hasunga aliwahakikishia wananchi kuwa mashindano hayo yatakuwa endelevu ili kutekeleza mpango mkakati wa uimarishaji na uboreshaji wa michezo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 ibara ya 161.
No comments:
Post a Comment