WAZIRI KAMWELWE ASISITIZA KUWAONDOA WAPANGAJI WASIOLIPA KATIKA NYUMBA ZA SERIKALI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 23 August 2019

WAZIRI KAMWELWE ASISITIZA KUWAONDOA WAPANGAJI WASIOLIPA KATIKA NYUMBA ZA SERIKALI


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akifafanua jambo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, kuhusu maamuzi ya Serikali katika utekelezaji wa madeni yanayodaiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kwa wadaiwa sugu mjini Dodoma.


WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesisitiza kuwa Wizara kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) itaendelea kuwaondoa wadaiwa sugu wa kodi ya pango za majengo na nyumba  za watumishi wa umma, wabunge na baadhi ya Taasisi za Serikali lengo likiwa ni kuimarisha Wakala huo ili uweze kujiendesha wenyewe na hatimaye kuweza kukamilisha miradi mingine inayoitekeleza.

Alisisitiza hayo katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu jijini Dodoma, wakati akijibu hoja iliyoibuliwa na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyetaka kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu suala hilo.

Aliongeza kuwa uamuzi huo wa kuwaondoa wadaiwa sugu unazingatia taratibu stahiki ambazo zinatambulika kisheria.

 “Wizara imeamua kufanya hivi kwa mujibu wa sheria kwani Wakala unadai wateja wake zaidi ya shilingi bilioni 20 hivyo tukiendelea kulimbikiza madeni haya, Wakala utashindwa kujiendesha na hatimaye kufa kabisa” alifafanua Waziri Kamwelwe.

Aidha, Waziri Kamwelwe, amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2018/19 Wakala huo umefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 19 kutoka vyanzo vyake vya ndani vya mapato na Wakala unatarajia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 114 katika mwaka wa fedha 2019/20.

Ameendelea kueleza kuwa hadi kufikia Juni, 2019 Wakala umekamilisha baadhi ya miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino iliyopo jijini Dodoma na ujenzi wa nyumba kwenye mradi wa kufufua umeme iliyopo Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Taasisi zilizo chini yake, wakiwa katika kikao kilichohusisha uwasilishaji taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kamati hiyo, mjini Dodoma.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa, wakati akiwasilisha taarifa ya sekta hiyo, Naibu Waziri huyo aliielezea kamati hiyo kuwa Serikali inaendelea kulipa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege hapa nchini na tayari bilioni 5.7 zimeshapokelewa Wizarani kwa ajili ya fidia ya Uwanja wa Ndege wa Dodoma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Selemani Kakoso, ameishauri Wizara kupitia Wakala huo kuhakikisha inaondoa kero na malalamiko ya wateja wake kwa kufanya maboresho ya nyumba zake.

Aliendelea kushauri kuwa Serikali iangalie namna ya kuwapatia Wakala  mfuko wa dharura kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyosimama hususani ile ambayo ipo katika hatua ya kuiongezea Serikali gharama kubwa kwa kutoendelea kwa ujenzi huo.

Kikao cha Kamati hiyo kimeshirikisha wajumbe mbalimbali ikiwemo Naibu Waziri wa Sekta ya Ujenzi  Elias Kwandikwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye na kinaendelea kupokea taarifa ya utekelezaji ya Sekta hiyo ambayo inatokana na maazimio ya vikao vya Bunge vilivyopita.

No comments:

Post a Comment