MSIMU UJAO MALIPO YA WAKULIMA WA PAMBA YAPITIE BENKI - MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 8 August 2019

MSIMU UJAO MALIPO YA WAKULIMA WA PAMBA YAPITIE BENKI - MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua pamba inayosubiri kuuzwa na wakulima kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Fresho Investment Company cha mjini Shinyanga Agost 9, 2019. Alikuwa katika ziara ya kukagua mwenendo wa uuzaji wa pamba. Kushoto ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Fred Shoo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua pamba inayosubiri kuuzwa na wakulima kwenye kiwanda cha kuchambua pamba cha Fresho Investment Company cha mjini Shinyanga Agost 9, 2019. Alikuwa katika ziara ya kukagua mwenendo wa uuzaji wa pamba. Kulia kwake  ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Fred Shoo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameagiza kwamba kuanzia mwakani malipo yote ya wakulima wa pamba yawe yanapitia benki ambapo wakulima wataingiziwa fedha kupitia akaunti zao.

Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwasihi wakulima wafungue akaunti katika benki mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao ili waweze  kufanikisha mkakati huo na pia kuhifadhi fedha zao kwa ajili ya matumizi ya baadae. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Agosti 8, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Luguru, wilayani Itilima mara baada ya kukagua ghala la pamba la Chama cha  Ushirika cha Msingi cha  Maendeleo.

Alitembelea kijiji hicho kwa lengo la kujionea mwenendo wa uuzaji wa zao la pamba katika Chama cha Msingi Maendeleo na alihakikishiwa kwamba kwa sasa uuzaji wa pamba unaendelea vizuri. Waziri Mkuu alisema ni vizuri malipo ya wakulima yapitie benki ili kuwawezesha kupanga matumizi mazuri ya fedha zao na pia watapa fursa ya elimu ya matumizi mazuri ya fedha.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alieleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika wilaya hiyo ukiwemo mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ambao umefikia asilimia 95.

“Jumla shilingi bilioni 1.5 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya inayojengwa eneo la Nguno, ambapo majengo yote saba ya kiupaumbele yamekamilika.”

Alisema mwaka 2017/2018 Serikali ilitoa sh. bilioni 2.34 kwa ajili ya miradi ya maji ya vijiji vya Lagangabilili, Mwamapalala, Kabale, Ikungulipu na Isengwa, yote imekamilika na inatoa maji. Alisema mwaka 2019/2020 Halmashauri hiyo kupitia RUWASA imetengewa sh. bilioni 4.84 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji. Mradi huo utavinufaisha vijiji 78. Awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Msingi cha Maendeleo Luguru na Itubilo, Buzo Hussein alimshukuru Waziri Mkuu kwani wakati wote amekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia kero mbalimbali zinazowakabili wakulima nchini na kuzitafutia ufumbuzi. 

“Hii yote inatokana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inayowataka viongozi kufuatilia changamoto za wananchi kwa vitendo na kuzitatua.”

Alisema katika ghala la chama chao kuna jumla ya kilo 175,235 za pamba ambazo zimekusanywa kutoka kwa wakulima ikiwa inasubiri wanunuzi.

WAZIRI MKUU AWAONYA MKURUGENZI NA MWEKAHAZINA SHINYANGA


WAKATI HUO HUO, Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Bw. Geoffrey Mwangulumbi pamoja na Mwekahazina wa Manispaa hiyo, Bw. Pascal Makoye kuwa anawataka wabadilike na waache kugombana na badala yake watekeleze majukumu yao ipasavyo.

Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Bibi Zainab Telack azisimamishe kazi kampuni zote zilizopewa zabuni ya kukusanya mapato katika Manispaa hiyo kwa kuwa zimeshindwa kufanya kazi vizuri na zina madeni.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo wakati alipozindua nyumba 10 za Askari Polisi katika Manispaa ya Shinyanga eneo la Kambarage. Mradi huo umetokana na fedha kiasi cha sh. milioni 225 zilizotolewa na Rais Dkt. John Magufuli.

Amesema viongozi hao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia kikamilifu zoezi la ukusanyaji wa mapato na kutoa kazi hiyo kwa kampuni zisizokuwa na uwezo. Amesema mwaka jana walikadiria kukusanya sh. milioni 800 na badala yake walikusanya sh. milioni 500.

Waziri Mkuu amesema Manispaa hiyo haiwezi kusonga mbele kimaendeleo iwapo viongozi wake hawaelewani wanagombana kila siku. “Mkurugenzi na wenzako nawaonya kwa mara ya mwisho badilikeni na hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu ipasavyo yakiwemo ya ukusanyaji wa mapato.”

Akizungumzia kuhusu nyumba za Askari Polisi, Waziri Mkuu amesema lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kuhakikisha askari wanaishi katika mazingira mazuri yatakayowawezesha kutekeleza vizuri majukumu yao. “Ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao lazima wawe na makazi mazuri”.

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa askari waliopewa funguo kwa ajili ya kuishi katika nyumba hizo wahakikishe wanazitunza vizuri na hata inapotokea wamehamishiwa kwenda katika vituo vingine, wale watakaohamia wakute nyumba hizo zikiwa katika mazingira mazuri.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa nyumba hizo ni endelevu, ambapo pia amezitaka idara mbalimbali za Serikali ziendelee na mchakato wa ujenzi wa nyumba zake kwani wakiwa na nyumba nyingi itasaidia kupunguza idadi kubwa ya askari wanaoishi uraiani.

Awali, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga ACP Richard Abwao alisema awali fedha zilizotolewa zilikuwa zijenge nyumba tisa za vyumba viwili lakini kutokana na ubunifu waliweza kuboresha mradi huo kwa kuongeza nyumba moja sambamba na kuongeza chumba kimoja, hivyo kuufanya mradi huo kuwa na nyumba 10 zenye vyumba vitatu vya kulala.

Pia alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa upendo wake mkubwa kwa Jeshi la Polisi Tanzania kwa kulipatia fedha za kuboresha makazi ya askari. Mradi huo umekamilika kwa gharama ya sh. milioni 278, 565, 500 wastani wa gharama za ujenzi kwa nyumba moja ni sh. milioni 27, 856, 550. Alisema kiasi cha nyongeza cha sh. milioni 53, 565,500 zilitolewa na wadau mbalimbali.


No comments:

Post a Comment