NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki amewahakikishia wawekezaji kutoka Marekani uwepo wa mazingira rafiki ya uwekezaji nchini kwa kuzingatia mchango wao katika masuala ya uwekezaji.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kongamano la siku moja la kujadili masuala ya kuboresha mazingira ya biashara pamoja na uwekezaji nchini lililofanyika tarehe 17 Juni, 2019 katika Ukumbi wa mikutano wa Hyatt Jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yaliyolenga kujadili changamoto zinazowakabili na kujadili namna bora ya kukabiliana nazo na hatua mahsusi ambazo Serikali imeendelea kuzichukua ili kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Kongamano hilo limeandaliwa na Ubalozi wa Marekani kwa kushirikiana na Chemba ya Wafanyabiashara wa Kimarekani nchini Tanzania na kuhusisha wawakilishi wa Kampuni 47 kati ya 238 za Kimarekani na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi, Maafisa Waandamizi wa Serikali ya Tanzania, Wawakilishi wa Ubalozi wa Marekani pamoja na Wanachama wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kimarekani.
Waziri Kairuki alieeleza nia ya Serikali ni kuendelea kuwa na mazingira wezeshi yanayowavutia wawekezaji nchini katika kuendelea kuchangamkia fursa zilizopo na kupokea maoni yao ili kutatua changamoto wanazokumbana nazo.
“Serikali itaendelea kuweka mkazo mkubwa wa maboresho katika maeneo mbalimbali yatakayo kuvutia wawekezaji ikiwani pamoja na uboreshwaji wa sekta ya mawasilino, miundombiu ya barabara na usafirishaji ili kuwa na mazingira mazuri ya wawekezaji kuja kuwekeza nchini,”alisema Waziri Kairuki.
Aliongeza kuwa ifikapo mwezi Julai mwaka huu, serikali itaanza kutekeleza Mpango Kazi wa Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji ambao tayari umefanyiwa maboresho na utekelezaji wake utaanza mapema mwaka ujao wa fedha wa 2019/ 2020.
Aidha waziri aliahidi kuendelea kusimamia maeneo muhimu ikiwemo ushiriki wa sekta binafsi katika maeneo ya uwekezaji na kueleza maboresho haya yatatekeleza hasa katika kuboresha mifumo na kuwa na maziringa mazuri yanayotabirika kwa wawekezaji.
“Kwa kutambua umuhimu wa Sekta binafsi, tutaendelea kusimamia ushiriki wao kikamilifu ili kuleta tija pasipo kubagua sekta hiyo na kuendelea kuwa na mifumo inayotabirika kwa ajili ya wawekezaji.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi alifafanua kuwa, jitihada za Serikali ni kuhakikisha kunakuwa na mahusiano mazuri ya kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili kwa kuzingatia zote zinategemeana katika masuala hayo ya uwekezaji.
“Kimsingi tunapaswa kuwa na uelewa wa pamoja kuwa, Tanzania na Marekani zinategemeana katika masuala haya ya uwekezaji kwani mnatuhijai na sisi tunawahitaji hivyo lazima tukae meza moja na kuyajenga endapo tunaona kuna maeneo ya kuboresha yenye tija ya kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo ni vyema tukayafanyia kazi pamoja”, Alisistiza Profesa Kabudi.
Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Marekani nchini Dk. Inmi Patterson katika hotuba yake ya ufunguzi alieleza kuwa, majadiliano hayo ni mwanzo mzuri wa kuendelea kutekeleza mabadiliko ya kisera yatakayosaidia kuongeza uwazi na mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara nchini.
“Majadiliano ya leo ni mwanzo wa utekelezaji wa mabadiliko ya kisera yatakayoongeza uwazi na kuboresha mazingira ya kufanya biashara na tunaunga mkono jitihada hizi za Serikali ya Tanzania kwa kuzingatia mahusiano mazuri yaliyopo sasa,”Alieleza Kaimu Balozi Patterson.
Aliongezea kuwa Serikali ya Marekani itaendelea kuunga mkono ushiriki wa sekta binafsi katika jitihada za maendeleo nchini humo kupitia ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma (Public private partnerships) ambao utaimarisha mazingira ya kibiashara na ubunifu ambao utanufaisha Wananchi wa Tanzania.
Aidha alieleza kuwa nchi yake imeendelea kuwa mstari wa mbele katika uwekezaji, kwa kuzingatia Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Wafanyabiashara wa Kimarekani wamewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 4.7 nchini Tanzania na kuzalisha takriban nafasi za ajira 52,000 katika kipindi cha miaka 28 nchini kote Tanzania.
No comments:
Post a Comment