Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na
wadau imedhamiria kuboresha huduma na upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu
wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa
hafla ya kupokea vifaa saidizi kwa ajili ya watu wenye ulemavu iliyoandaliwa na
Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista
Mhagama alisema kuwa kundi la Watu wenye Ulemavu lilikosa baadhi ya fursa hapo
awali kutokana na changamoto ambazo wamekuwa wakikabiliana nazo.
“Tunafahamu watu wenye
ulemavu wanauhitaji wa huduma bora na vifaa saidizi vitakavyo wawezesha kumudu
mazingira ili nao waweze kujumuika katika nyanja zote,” alisema Mhagama
Alifafanua kuwa
takwimu na Sensa ya Taifa ya Watu wenye na Makazi ya mwaka 2012, imekadiria
idadi ya watu Tanzania ni zaidi ya milioni 44 ambapo milioni 2.5 ni Watu wenye
Ulemavu.
Waziri Mhagama
alisema, Serikali imeazima kuboresha huduma kwa Watu wenye ulemavu ikimemo
kutoa elimu bure na kuimarisha elimu jumuishi, kujenga vituo vya afya na
hospitali pamoja na utoaji wa matibabu bure kwa watu wenye ulemavu wasio na
uwezo.
Mbali na hayo,
alihimiza wadau pamoja na makampuni kuona umuhimu wa kuhudumia kundi la watu
wenye ulemavu wakiwa wanatoa huduma mbalimbali za kijamii.
Aidha, alipongeza
Kampuni ya Singara Tanzania (TCC) kwa msaada huo na kuwashauri waendelee
kukumbuka kundi hilo.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa TCC, Bw. Godson Killiza alisema kuwa watu
wenye ulemavu wana uwezo mkubwa na nijukumu kama wadau kuwasaidia na kuwaunga
mkono kwenye masuala mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa
Shirikisho la Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bi. Ummy Nderiananga alieleza
kuwa juhudi za Serikali katika kushirikiana na wadau itasaidia kwa kiasi
kikubwa kuondoa changamoto za Watu wenye Ulemavu katika kufanikisha masuala
yao.
No comments:
Post a Comment