Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga,
akisikiliza na kunukuu hoja za Makandarasi wa ndani katika kikao cha Katibu
Mkuu huyo na makandarasi hao kilichofanyika jijini Dodoma.
Makandarasi wa ndani
kutoka katika mikoa mbalimbali nchini wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, katika kikao
cha Katibu Mkuu huyo na makandarasi hao kilichofanyika jijini Dodoma.
Na
Siti Said
SERIKALI kuptia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) imesema kuwa ina mpango wa kuwajengea uwezo makandarasi wa ndani ili waweze kutekeleza kazi zao na kuongeza ushindani katika soko la ajira.
Hayo yamesemwa na
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Arch. Elius Mwakalinga, jijini Dodoma wakati
akifungua kikao kilichoshirikisha wakurugenzi wa Wizara na Taasisi zake pamoja
na makandarasi kutoka katika mikoa mbalimbali nchini.
Katibu Mkuu huyo,
amesema kuwa Serikali kupitia Wizara yake itaanza kuwawezesha makandarasi hao
kwa kuwashirikisha kwenya miradi michache mikubwa ya Wizara inayojengwa na
makandarasi wa nje ili kupata taaluma na ujuzi kutoka kwao.
“Nimeamua kuitisha
kikao hiki ili kuwaeleza mikakati ya Serikali ya kuwajengea uwezo na kujadili
kwa pamoja changamoto zenu na hatimae kuzitafutia ufumbuzi”, amesema Katibu
Mkuu Mwakalinga.
Aidha, amefafafanua
kuwa mkakati huo umeanza ndani ya Wizara kwa kuwapeleka watumishi 44 kwenye miradi
nane ya ujenzi inayotekelezwa nchini ikiwemo mradi wa daraja la Selander ambapo
watumishi hao watashiriki mwanzo hadi mwisho wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Ameongeza kuwa lengo
la kufanya hivyo ni kupata wataalamu wazalendo katika miaka ijayo ili nao kutoa
elimu walioipata kwa wenzao na hatimaye kupata wataalamu wengi wazalendo
watakaosaidia kukuza uchumi wa nchi na kulinda maslahi mapana ya Taifa.
Kwa upande wake,
Mhandisi Oscar Lisi kutoka mkoani Mwanza, amemuomba Katibu Mkuu Mwakalinga kuwa
mkali na kuchukua hatua katika suala la rushwa kwani amesema kuwa sekta hiyo
haiendelei na haikui kutoka na kuingiliwa na rushwa.
Pia mkandarasi huyo ameiomba
Serikali kulegeza masharti yaliyomo kwenye mikataba ya zabuni kwani masharti
mengi yanaonekana kumnyima fursa mkandarasi wa ndani katika zabuni
zinazotangazwa na Serikali.
Naye, Mhandisi kutoka
Mbeya, Shakira Kiwanga, amemuomba Katibu Mkuu Mwakalinga, kuwasaidia kuzungumza
na mabenki ili kuweza kupata mikopo ambayo itasaidia kuinua na kukuza mitaji
yao kwani wengi wao wana hali duni.
Mkutano huo
umeshirikisha Makandarasi kutoka mikoa mbalimbali nchini lengo likiwa ni kupata
taarifa na mikakati ya Serikali kuhusu taaluma yao.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment