NMB YATOA FURSA KUWEKEZA HATI FUNGANI YENYE FAIDA NDANI YA MUDA MFUPI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 10 June 2019

NMB YATOA FURSA KUWEKEZA HATI FUNGANI YENYE FAIDA NDANI YA MUDA MFUPI

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi  wa Benki ya NMB, Omari Mtiga (katikati) akizungumza na wanahabari wakati wa ufunguzi wa hati fungani za benki hiyo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja mwandamizi wa wateja wa amana, Isaac Mgwassa pamoja na Meneja Mwandamizi wa Ushauri NMB, Sigifrida Joseph (kushoto).

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi  wa Benki ya NMB, Omari Mtiga (kushoto) akifafanua jambo kwa wanahabari (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa hati fungani za benki hiyo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja mwandamizi wa wateja wa amana, Isaac Mgwassa akifuatilia.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi  wa Benki ya NMB, Omari Mtiga (katikati) akimsikiliza Meneja mwandamizi wa wateja wa amana, Isaac Mgwassa alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa mauzo ya hati fungani za NMB leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja Mwandamizi wa Ushauri NMB, Sigifrida Joseph pamoja na Meneja mwandamizi wa wateja wa amana, Isaac Mgwassa (wa kwanza kulia).

BENKI ya NMB leo imetangaza hati fungani 'NMB Bond' itakayozalisha riba ya asilimia 10 kwa mwananchi yeyote atakayewekeza katika benki hiyo.
Hii inakuwa mara ya pili kwa Benki ya NMB kutoa hati fungani ambayo itapatikana katika matawi yote ya benki hiyo huku kiasi cha chini kupata fursa hiyo kikiwa shilingi 500,000/-.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Omari Mtiga alisema benki hiyo imefungua fursa hiyo baada ya kupata kibali cha kutoka kwa Mamlaka ya Masoko ya Mtaji nchini (CMSA).

Akifafanua zaidi Bw. Mtiga alisema wawekezaji wa hati fungani hiyo kwa sasa watapata riba ya asilimia 10 kwa mwaka itakayokuwa ikilipwa kila baada ya miezi mitatu kwa miaka mitatu, yaani mpaka Juni mwaka 2022.

"Hati fungani ya NMB inauzika pia na mteja anaweza kuiuza kwa mteja mwingine na kupata fedha yake kabla ya kukomaa kwa hati fungani yaani miaka mitatu. Wawekezaji wanaweza kuiuza hati fungani hiyo kabla ya kukomaa katika soko la wazi kupitia mawakala wa soko la mitaji kwa kufuata misingi ya soko la hisa la Dar es Salaam," alisema Bw. Mtiga.

Alisema msingi wa Benki ya NMB ni uwekezaji wa fedha kwa wateja wadogo licha ya uwepo wa njia nyingine za kutunisha mfuko kwa hati fungani ya NMB. Aliongeza benki hiyo inategemea kutunisha mfuko kwa shilingi bilioni 25 huku ikiwa na fursa ya kuongeza hadi kufikia bilioni 40.

Aidha Meneja Mwandamizi wa Wateja wa Amana wa Benki ya NMB, Isaack Mgwasa alibainisha kutokana na matokeo ya hati fungani iliyopita kufanya vizuri benki hiyo imetumia fursa hiyo muhimu kukidhi kiu ya wateja wao jambo ambalo linakuza na kuendeleza soko la mitaji nchini.

"...Sisi kama benki tumeona umuhimu kuchangia kwa kiwango kikubwa katika kuendeleza masoko ya mitaji na pia kupigania elimu ya fedha kwa jamii. Hati fungani hii mpya itaanza kuuzwa Juni 10, 2019 mpaka Julai 8, 2019 na riba itaanza kulimbikizwa kuanzia tarehe hiy," alifafanua Bw. Mgwasa.

No comments:

Post a Comment