SERIKALI YA UJERUMANI KUENDELEA KUISAIDIA JWTZ, YAAHIDI KUJENGA HOSPITALI YA KIJESHI DODOMA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 9 May 2019

SERIKALI YA UJERUMANI KUENDELEA KUISAIDIA JWTZ, YAAHIDI KUJENGA HOSPITALI YA KIJESHI DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Dk. Detlef Waechter mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Dk. Detlef Waechter mara baada ya mazungumzo yao pamoja na Ujumbe kutoka nchini Ujerumani Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Dk. Detlef Waechter mara baada ya kumaliza kikao chao  na ujumbe kutoka nchini Ujerumani Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli akisalimiana na Malte Loknitz kutoka Ujerumani (kushoto) ambaye alikuwa akitambulishwa na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Dk. Detlef Waechter katikati mara baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mjumbe kutoka nchini Ujerumani Malte Loknitz akizungumza na vyombo vya habari kwa lugha ya Kiswahili mara baada ya kikao chao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mjumbe kutoka nchini Ujerumani Malte Loknitz mara baada ya kuzungumza na vyombo vya habari Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU.
SERIKALI ya Shirikisho la Ujerumani kupitia Mpango wa Kusaidia Majeshi Rafiki imekubali kuongeza kipindi cha kutoa misaada kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa miaka 4 zaidi kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 ambapo pamoja na mambo mengine itajenga Hospitali kubwa ya Kijeshi yenye kiwango cha “Level 4” Mkoani Dodoma.
Balozi wa Ujerumani hapa nchini Mhe. Dk. Detlef Wäechter akiwa na ujumbe kutoka Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani ametangaza uamuzi huo Mei 9, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Pamoja kujenga hospitali hiyo Mhe. Dk. Wäechter amesema katika ushirikiano huo Ujerumani kupitia Timu ya Ushauri ya Wataalamu wa Kijeshi (GAFTAG) itaongeza mafunzo na vifaa vya ulinzi wa amani, itaendelea kufundisha madaktari wa Jeshi na kutoa vifaa vya matibabu na kutoa mafunzo ya ulinzi wa amani.
Katika ushirikiano wa sasa utakaoishia 2021, kati ya mwezi Juni 2017 na Machi 2019, Ujerumani imejenga Hospitali ya Kanda huko Monduli Mkoani Arusha ambayo imewekewa vifaa tiba vinavyotumia teknolojia ya kisasa na itakayotumiwa kama Hospitali ya Rufaa ikisaidiana na Hospitali ya Kijeshi ya Lugalo iliyopo Jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa hospitali hiyo umegharimu shilingi Bilioni 5 na Milioni 947 ambapo shilingi Milioni 346.8 kati yake zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Ufadhili mwingine uliotolewa ni upanuzi na uboreshaji wa Chuo cha Sayansi na Tiba cha Lugalo, ujenzi wa karakana za Jeshi katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga na Mwanza, ujenzi wa idara ya dharura ya Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, ujenzi wa mabweni ya wanafunzi katika Hospitali ya Kanda iliyopo Bububu - Zanzibar, uboreshaji wa Hospitali za Kanda zilizopo Zanzibar, Mbeya, Mwanza na Tabora, msaada wa magari na vifaa tiba.
Mhe. Rais Magufuli ameishukuru Ujerumani kwa kuendeleza na kuukuza uhusiano na ushirikiano na Tanzania na amemhakikishia Mhe. Balozi Wäechter kuwa Serikali ya Tanzania itahakikisha misaada yote inayotolewa inaleta manufaa yaliyokusudiwa.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Mabeyo na Katibu wa Kwanza wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Bw. Malte Loknitz aliyeongoza ujumbe wa Maafisa kutoka Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani pamoja na Mshauri wa GAFTAG hapa nchini Luteni Kanali Thomas Nalbach.

No comments:

Post a Comment